
MAWAKILI wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC wameanza kutoa mawasilisho ya kupinga kesi ya kutaka matokeo ya uchaguzi wa urais kufutiliwa mbali kama inavyoombwa katika kesi ya kupinga matokeo hayo ya upande wa Raila Odinga na Martha Karua.
Wakili wa tume hiyo Githu Muigai amesema IEBC iliandaa uchaguzi wa mujibu wa sheria na katiba za nchi na mwenyekiti wake Wafula Chebukati ni mwathiriwa wa ‘tetesi za wongo,madai yasiyo na ushahidi na uvumi.
Muigai amesema endapo uchaguzi uliokamilika haukuwa wa uwazi basi nyadhifa nyingine zote ambazo zilizowania katika uchaguzi ambao IEBC iliendesha zinafaa kutajwa kama zenye kasoro.
Muigai aliiambia mahakama ya juu kwamba miongoni mwa mawakili wa upande wa mlalamishi kunao waliochaguliwa katika uchaguzi huo kama magavana ,maseneta na wabunge na wanafaa kuulizwa iwapo uchaguzi wao pia ulikumbwa na kasoro.
Jana upande wa walalamishi kupitia mawakili wao uliwasilisha maombi,ushahidi na masuala waliotaka mahakama kuzingatia na kufutilia mbali matokeo hayo ya uchaguzi.
KESI YA KUPINGA USHINDI WA RUTO KITI CHA URAIS INAENDELEA KUSIKILIZWA MAHAKAMANI KENYA…