
MAKOCHA wa Yanga SC na Azam FC, wameweka wazi kuwa wanazitaka pointi tatu kwenye mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Ikumbukwe kwamba, Yanga haijafungwa kwenye ligi tangu msimu wa 2020/21 ilipofungwa 1-0 dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Mkapa, Aprili 25,2021 kwa bao la Prince Dube.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema wapo tayari kuikabili Azam FC na wanawaheshimu wapinzani wao ila wanahitaji pointi tatu.
“Tulikuwa na muda mfupi wa maandalizi kwa ajili ya msimu mpya ila kutokana na mapumziko ambayo yalipatikana hivi karibuni tumeyatumia vizuri kufanya maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC pamoja na mechi nyingine.

“Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu, tumewaambia wachezaji kuwa ni lazima wajitume, wajitahidi na wasilewe sifa na tunajiandaa kupata ushindi kwenye kila mchezo,” alisema Nabi.
Kocha wa Azam FC, Kali Ongala ambaye ni maalumu kwa ajili ya kuwanoa washambuliaji kikosini hapo, alisema wanatambua ubora wa Yanga kwa miaka miwili ila watajitahidi kuwa bora kila mahali.
“Tunajua Yanga imekuwa bora kwa miaka ya hivi karibuni ila tupo tayari na ni wachezaji watatu ambao watakosekana kwenye mchezo huo ikiwa ni Ismail Kader, Rodgers Kola na Keneth Muguna,” alisema.
Yanga imecheza mechi mbili na kushinda zote ikiwa nafasi ya pili na pointi sita, inakutana na Azam FC iliyoshinda mechi moja na kukusanya pointi nne msimu huu.
WAANDISHI: ALU HAMIS, JOSEPH PAMBAU, DARLING GULAMU NA LUNYAMADZO MLYU
YANGA NA TFF KUNA JAMBO? ISHU YA KISINDA YAIBUA SURA MPYA | KROSI DONGO