
MASHABIKI wa Manchester United wakasirishwa na kiwango cha kiungo wao mkabaji Casemiro ambae alionesha kiwango duni siku ya jana katika mchezo dhidi ya Real Sociedad ambapo Manchester United walipoteza mchezo kwa 1-0.
Kocha mkuu wa Manchester United Erik ten Hag alifanya mabadiliko sita katika mchezo wa jana kutoka kikosi kilichoishinda dhidi ya Arsenal siku ya Jumapili. Cristiano Ronaldo, Harry Maguire na Victor Lindelof walikuwa miongoni mwa waliopewa nafasi hiyo.

Mchezaji mwingine aliyepewa nafasi ya kuanza na Ten Hag alikuwa Casemiro. Alicheza dakika zote 90 kwa mara ya kwanza tangu uhamisho wake wa pesa nyingi kutoka Real Madrid majira ya joto, kiungo huyo wa kati wa ulinzi alikuwa ni nguzo muhimu katika kikosi Real Madrid kilichoshinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini kutokana na uchezaji bora wa Christian Eriksen na Scott McTominay, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil amelazimika kusubiri nafasi yake.
Casemiro alipewa nafasi siku ya jana dhidi ya Sociedad, lakini alishindwa kutamba kwenye mechi hiyo. Casemiro alikuwa akipoteza mipira kiwepesi na hakuendana na kasi ya mchezo.

Baada ya mpira kumalizika mashabiki wa Manchester United walienda kwenye mitandao ya kijamii kuelezea wasiwasi wao juu ya uchezaji wa Casemiro.
Wengi walitarajia nyota huyo wa zamani wa Real Madrid angeingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Ten Hag, lakini kiwango bora cha McTominay kilifuta mipango hiyo.
Imeandikwa na: John Mbwambo kwa msaada wa mitandao