
PAZIA la michuano ya kimataifa ile inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa msimu huu 2022/23 kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho lilifunguliwa jana Ijumaa lakini leo Jumamosi na kesho Jumapili ndiyo timu za hapa nyumbani zitaanza kutupa karata zake.
Ikumbukwe kuwa kwa msimu huu Tanzania ina wawakilishi wanne katika michuano hiyo ambapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika zipo timu za Simba na Yanga wakati kwenye Kombe la Shirikisho zipo Azam FC na Geita Gold.
Katika timu hizo ni Azam FC pekee ambao hawatacheza wikiendi hii kwa kuwa hawataanzia hatua ya awali ya michuano hiyo kama Simba, Yanga na Geita Gold ambao wenyewe watakuwa na kibarua cha kupambana katika mechi ili wafuzu hatua inayofuata.
Leo Jumamosi Simba na Yanga, wenyewe watakuwa na vibarua vya kufanya mbele ya wapinzani wao wakati Geita watacheza kesho Jumapili. Hapa Championi Jumamosi linakuchambulia kwa undani kuhusiana na michezo hiyo miwili ya leo.

NYASA BIG BULLETS V SIMBA
Wawakilishi wa kwanza wa nchi ni Simba ambao wenyewe watacheza na Nyasa Big Bullets katika Uwanja wa Taifa wa Malawi, Bingu nchini Malawi wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 41,100.
Hii ni mechi ngumu kwa Simba kwa kuwa mara nyingi kwenye mashindano haya mcheza kwao hutunzwa. Ingawa Big Bullets wanaonekana kama timu ya kawaida lakini inawapasa Simba kuwa makini kwa kuwa hawa ni mabingwa wa Malawi na timu ambayo ina mashabiki wengi nchini humo.
Makali ya timu hii ni kupata ushindi wa mabao mengi kwenye mechi zake na wamekuwa wazuri sana wa kutumia nafasi pale ambapo wanapopata.
Kikosi hicho kwa sasa kipo mikononi mwa Kocha Mganda, Kalisto Pasuwa na ametengeneza timu ya hatari ambayo kwa asilimia 99 inaundwa na wachezaji wazawa wa nchi hiyo huku wakiwa na mchezaji mmoja pekee kutoka Nigeria, Babatunde Adepoju.
Big Bullets ambao msimu uliopita kwenye mashindano haya walitolewa hatua ya kwanza wanajivunia safu yao ya ushambuliaji ambayo imekuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi kila mara inapopata nafasi.
Simba wenyewe wamekuwa na timu yenye mchanganyiko wa wachezaji akiwemo Peter Banda ambaye anatokea hapohapo Malawi na mchanganyiko huo umeisaidia timu hiyo kufanya vizuri ndani ya misimu minne iliyopita.
Mshindi wa jumla wa mechi hii atacheza na mshindi wa mchezo kati ya Red Arrows ya Zambia au Agusto ya Angola.
WALIPOISHIA MSIMU ULIOPITA
Timu zote mbili zilikuwepo katika mashindano haya msimu uliopita lakini wote hawakufanya vizuri. Big Bullets wao waliondoshwa hatua ya awali wakati Simba waliondoshwa hatua ya kwanza na kutinga Kombe la Shirikisho.
MAFANIKIO YAO MAKUBWA
Katika mashindano haya mafanikio makubwa kwa Big Bullets ni kufika hatua ya makundi mwaka 2004.
ZALAN V YANGA
Yanga ni wawakilishi wengine wa Tanzania katika mashindano haya ambapo wenyewe watacheza na Zalan FC na mechi yao ya kwanza itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambao uliombwa na wapinzani wao.
Kucheza katika uwanja huo ni faida kubwa kwa Yanga kwa kuwa watacheza mbele ya mazingira ambayo wanayajua vilivyo.
Zalan ambao ndiyo wenyeji wa mchezo huu wenyewe walianzishwa mwaka 1998 na wamepata nafasi ya kuingia Ligi ya Mabingwa baada ya kubeba ubingwa wa Ligi ya Sudan Kusini.
Wenyewe hawaonekani kuwa na makali kuwazidi wapinzani wao ambao wamekuwa na kikosi kizuri kutokana na usajili ambao wameufanya.
Yanga wana hasira ya kufanya vizuri kwa msimu huu baada ya kufanya vibaya msimu uliopita ambao waliishia hatua ya awali baada ya kuondolewa na Rivers United ya Nigeria kwa kufungwa nyumbani na ugenini.
Silaha kubwa wanayoitegemea Yanga ni aina ya wachezaji wake ambao wengi wao wana uzoefu mkubwa na mashindano haya akiwemo Stephane Aziz Ki, Bernard Morrison, Khalid Aucho, Yannick Bangala na Fiston Mayele.
Mechi hii ya kwanza na ile ya marudio zote zitapigwa katika uwanja huo na mshindi wa jumla ataenda kukutana na moja ya timu kati ya St. George ya Ethiopia au Al Ahli Tripoli ya Libya.
Mwandishi Wetu