
TAKRIBANI watu 11 wameuawa wakiwemo Maafisa wa Polisi nane na raia wanne katika maeneo yenye ukame yaliyopo Kaskazini mwa Kenya.
Polisi wa Kenya wametoa taarifa hiyo Septemba 25, 2022 na kueleza kuwa tukio hilo limetokea Septemba 24, mwaka huu huku wakibainisha kuwa shambulio hilo limetekelezwa na wezi wa mifugo.
Maafisa wa Polisi waliouawa walikuwa wakiwatafuta watu wa kabila la Pokot ambao walikuwa wamevamia kijiji na kuiba ng’ombe kisha kukimbia nao.
Wizi wa mifugo, migogoro ya ardhi na vyanzo vya maji ya malisho ya mifugo ni jambo la kawaida katika maeneo ya wafugaji yaliyopo Kaskazini mwa Kenya.
Mnamo Novemba, 2012 maafisa wa polisi 42 waliuawa katika shambulio la kuvizia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika eneo la Baragoi lililopo Kaskazini mwa Kenya.
Ililpofika Agosti, 2019 watu 12 waliuawa na wezi wa mifugo wanaoshukiwa kuwa Waethiopia wa kabila la Borana huko Kaskazini mwa Kenya.

Hayo yamejiri baada ya misimu minne mfululizo ya uhaba wa mvua kusababisha hali ya ukame ambapo mito na visima vilikauka na kuua zaidi ya ng’ombe milioni 1.5 nchini Kenya.
Mamlaka ya Hewa la Kitaifa ya nchi hiyo imeonya juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa migogoro ya kibinadamu na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao