
MAREKANI imetangaza msaada mwingine wa kiasi cha fedha cha Dola Milioni 625 kwa nchi ya Ukraine ili kiweze kuwasaidia katika vita dhidi ya Urusi.
Katika msaada huo Marekani imeadhimia kusaidia upatikanaji wa zana za kivita, ikiwemo makombora ya masafa marefu ya HIMARS. Huku kwa upande wa Urusi taarifa zikibainisha kuwa kitendo hicho ndiyo kwanza kinachochea kuendelea kwa vita kupamba moto.

Aidha Rais wa Marekani Joe Biden ameongea na Rais mwenzake Volodymyr Zelensky siku ya jumanne ambapo Ukraine imeendelea na mashambulizi yake makali dhidi ya vikosi vya Urusi katika maeneo ya Kusini na Mashariki mwa nchi hiyo ambapo wanafanya kazi ya kukomboa vijiji ambavyo vilichukuliwa na Urusi mapema vita ilipoanza Februari 24 mwaka huu.

Rais Biden ambaye aliungana na Makamu wake Harris Kamala walisisitiza juu ya lengo la Marekani kuwa itaendelea kuisaidia Ukraine kwa kila namna kwa muda wote katika juhudi zake za kupambana na ukandamizwaji wa uhuru wa nchi yake kutoka kwa Urusi.