
IMEELEZWA kwamba, Rais wa Heshima wa Simba SC, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameahidi kiasi cha shilingi milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo pindi wakiifunga Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola, leo Jumapili.
Hiyo imekuja ikiwa leo Jumapili Simba itakuwa na kibarua ugenini kucheza dhidi ya wenyeji wao hao ukiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.
Mchezo huo ambao utachezwa kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, utapigwa katika Dimba la 11 de Novembro. Marudiano ni Oktoba 16, mwaka huu Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Chanzo chetu kutoka Simba, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, kufuatia ugumu wa mchezo huo wa ugenini, tayari uongozi umeahidi kutoa zaidi ya shilingi milioni 200 kama sehemu ya bonasi ya ushindi.
“Hadi muda huu, sina shaka hata kidogo na ushindi wa ugenini, maana tayari uongozi umetangaza dau nono la hamasa kwa wachezaji, kuna uwezekano wa kila mchezaji kulamba zaidi ya shilingi milioni 10, kama watashinda, jambo ambalo limeongeza hamasa ya mapambano ugenini,” kilisema chanzo hicho.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amebainisha hilo kwa kusema: “Ni ukweli uliowazi kuwa, sisi kama klabu tayari tulishapanga kuhakikisha tunatoa bonasi nono katika kila mchezo wa ugenini wa Ligi ya Mabingwa.
“Tunakwenda kimataifa kucheza na wapinzani ambao tunawaheshimu, lakini mpango wetu ni kuanza ushindi ugenini, kisha tukirudi nyumbani tunamaliza kazi ili tutinge hatua ya makundi.
“Kuhusu ahadi zetu kwa wachezaji hilo wanajua kama wakishinda ugenini kimataifa wanapata kiasi gani na wakipata sare wanafahamu kiasi wanachopata.
“Hivyo ili kupata milioni 800, wanapaswa kushinda ugenini, au kuzipata milioni 600, basi wapate sare, hilo ni suala ambalo lipo kwenye mikataba yao, wanafahamu.”