
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Ahmed Ally leo Oktoba 12, 2022 amesema kikosi cha Primeiro de Agosto ya Angola kitatua Tanzania Oktoba 14, 2022 kuikabili Simba Jumapili katika Uwanja wa Mkapa katika mechi ya marudiano ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo wa awali Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini.
Ameongeza kuwa kikosi kimeanaza mazoezi rasmi jana tayari kuwavaa Waangola Jumapili “Kikosi chetu kimerejea rasmi mazoezini baada ya juzi kurejea kutokea Angola kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja wetu wa Mo Simba Arena na leo kitaingia kambini.”
“Tulishinda lakini bado hatujafuzu, safari hii hatutaki kurudia makosa. Tumeweka nguvu kubwa kuona kwamba mchezo wa jumapili tunapata matokeo mazuri ili tuingie makundi. Tumemiss kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
“Tutaendelea kuwakosa Shomari Kapombe ambaye sasa anaendelea kufanya mazoezi akiwa hospitali, ataukosa mchezo wa jumapili lakini michezo itakayofata atakuwepo. Jimmyson Mwinuke pia tutamkosa, taarifa njema ni Peter Banda amerejea kikosini.”
“Wageni wetu Primeiro de Agosto watawasili nchini Oktoba 14 majira ya mchana, kwa wale ambao wangependa kwenda kuwapokea wanakaribishwa uwanja wa ndege. Waamuzi wanatokea Afrika Kusini na watawasili nchini siku hiyo hiyo ya Oktoba 14.”
“Upande wa hamasa tunaendelea kupita kwenye vyombo vya habari na kupita mitaani, siku ya ijumaa tutakuwa Temeke, tutazunguka na kispika twende tukaiunge mkono timu yetu. Tukio la kipekee tutakuwa na chakula cha pamoja, biryan la kwenda hatua ya makundi.”
“Kwa wale ambao wana maflashflash ya kuwakawaka wanaruhusiwa kuja nayo muhimu liwe jekundu ili kuendana na rangi yetu.”
“Tiketi zinaendelea kununuliwa lakini bado kasi ni ndogo, tunajua asili yetu Watanzania ni kununua siku za mwisho, tunategemea manunuzi yatakuwa makubwa kuanzia kesho. Siku ya mchezo tutauza pia tiketi uwanjani. Tunasisitiza watu kununua mapema.”
“Kwa anayetaka kununua Platinum muda ni sasa mpaka naingia hapa zilikuwa zimebaki kama 20 hivyo inabidi kuwahi mapema kabla hazijaisha.”
“Tutaingia kwenye mchezo tukijua haujaisha, bado tunajua tunatakiwa kupambana kwa dakika zingine 90. Mechi haijaisha.”
Kuhusu Kocha Juma Mgunda Ahmed amesema kuwa kwa jinsi timu inavyocheza viziuri na kupata matokeo anaamini Bodi itafanya maamuzi sahihi.
“Kocha Mgunda anafanya vizuri na kila mmoja anaona. Simba tuliyokuwa tunaitaka tunaiona kwake. Namna watu wanashambulia, wanavyokaba na mpira unavyotembea. Bodi ya Wakurugenzi itafanya maamuzi lakini ametupa tunachotaka na tunaamini atatupeleka makundi.”
“Kila shabiki wa Simba afanye kila anachoweza yeye binafsi kuja uwanjani na muhimu zaidi kuhamasisha wenzake kuja uwanjani. Lengo letu ni kuingia makundi tukiwa watu wasiopungua 60,000.” amesema Ahmed Ally