
Watanzania Ibrahim Ramadhan na Fadi Ramadhan almaarufu Ramadhan Brothers, waliong’ara katika mashindano ya Australia’s Got Talent yaliyofanyika usiku wa Jumapili, Oktoba 16, 2022, wamefunguka mambo mengi kuhusu maisha yao ikiwemo jinsi walivyoanza sarakasi.
Ramadhan Brothers wamesema walianza sarakasi tangu wakiwa watoto wadogo lakini walikuwa wakicheza mitaani mpaka walipokuja kugunduliwa vipaji vyao na kocha wao ambaye ndiye aliyewaunganisha kimataifa.
Ramadhan Brothers wameshinda ngazi ya Golden Buzzers ambayo huheshimika duniani kote katika michezo mbalimbali na wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka washindi katika fainali zinazotarajiwa kumtoa mshindi mwezi ujao nchini Australia.
“Nawapongeza wanangu Ibrahim na Fadi (Ramadhan Brothers) kwa kipaji na ubunifu wenu wa kucheza sarakasi. Onesho lenu kupitia kipindi @GotTalentAU limeitangaza vyema nchi yetu ya Tanzania na nawatakia kheri katika kuendeleza sanaa yenu na kushiriki katika maonesho mbalimbali.”- Rais Samia Suluhu Hassan.