
FISTON Mayele, mshambuliaji wa Yanga, amesema kushindwa kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, sio mwisho wa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Juzi Jumapili, Yanga ilitolewa na Al Hilal kwa jumla ya mabao 2-1, sasa imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Spoti Xtra, muda mfupi baada ya msafara wa Yanga kurejea Dar ukitokea Sudan, nyota huyo amesema bado wana nafasi ya kufanya vizuri kimataifa.
“Tumeshindwa kufikia malengo ya kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, hatujapenda ila tuna nafasi katika Kombe la Shirikisho Afrika, huko tutapambana kufanya vizuri.
“Tulijadili na wachezaji baada ya mchezo tukakubaliana kwamba bado tuna kazi ya kufanya Kwa ajili ya mashabiki na kutimiza malengo kwani mashabiki wanahitaji ushindi Jambo ambalo nasi tunalihitaji pia. Hatujakata tamaa,” alisema Mayele.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alisema: “Makosa tutafanyia kazi ili kuwa bora na tunaamini kuwa tutafanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambako nako ni mashindano ya kimataifa.”
Kiungo wa Yanga, Bernard Morrison, alisema: “Tulijipanga kwa ajili ya kushinda, lakini haikuwa hivyo, tumepoteza lakini bado tupo kwenye mashindano ya kimataifa, hatujatolewa moja kwa moja.”
STORI; LUNYAMADZO MLYUKA