
TAKRIBANI watu 60 wameuawa katika maandamano ya kupinga serikali ya Chad ambapo kulitokea vurugu baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi hadharani.
Usiku wa kuamkia Oktoba 20, 2022 Serikali ya Chad ilitangaza amri ya kutotoka nje baada ya kutokea makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga utawala wa kijeshi kuongeza madaraka.
Mamia ya waandamanaji walijitokeza katika Mji mkuu wa N’Djamena na Moundou kwa ajili ya kuadhimisha tarehe ambayo awali watawala wa kijeshi walikuwa wameahidi kukabidhi madaraka.

Picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha waandamanaji wakichoma matairi moto huku moshi mweusi ukisambaa juu na kuweka vizuizi kwenye baadhi ya maeneo.
Wakati maandamano hayo yakiendelea walionekana watu waliovaa nguo za kiraia wakiwa kwenye magari yenye rangi nyeusi wakiwafyatulia risasi kwa waandamanaji.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la RFI, miili ya watu
18 ilionekana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Taifa na miongoni mwa watu waliouawa alikuwepo Mwandishi wa Habari wa kituo cha redio cha CEFOD, Oredjé Narcisse.
Shirika hilo limesema kuwa kuna baadhi ya familia zilienda katika hospital hiyo kwa ajili ya kuchukua miili ya ndugu zao lakini walirushiwa mabomu ya kutoa machozi.
Maafisa wa Polisi na wanajeshi wametumwa kwenda kutuliza ghasia huku milio ya risasi za moto ikisikika katika maandamano hayo.

Hayo yamejiri baada ya kiongozi wa muda Mahamat Idriss Deby kutangaza kuongeza miaka miwili zaidi ya utawala wake.
Ufaransa, Umoja wa Afrika na mataifa mengine yamelaani ukandamizaji wa vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao
idi ya waandamanaji hao.