
WATU 132 wamefariki dunia baada ya daraja linalotumiwa na waenda kwa miguu kuvunjika katika Jimbo la Guarajat lililopo Magharibi mwa India.
Waziri wa Nchi, Wizara ya Kazi na Ajira, Brijesh Merja amesema kuwa zaidi ya watu 80 wameokolewa katika daraja hilo ambapo wakati likipasuka kulikuwa na watu 400.
Picha za video zilizosambaa mitandaoni zilionesha mamia ya watu waliotumbukia katika Mto Macchu uliopo Mji wa Morbi, wakipiga kelele za kuomba msaada huku wengine wakining’inia kwenye kingo za daraja lililokuwa likizama mtoni.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya daraja hilo lililojengwa tangu enzi za ukoloni katika karne ya 19 kufunguliwa tena, kufuatia ukarabati uliokuwa ukifanywa hivi karibuni.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 230 ambalo limejengwa wakati wa utawala Uingereza ni maarufu kama kivutio cha utalii katika eneo hilo.
Mashuhuda mbalimbali wamesema kuwa watoto wengi walikuwa kwenye daraja hilo wakati likikatika na kusababisha wengine kutumbukia kwenye maji ambapo baadhi yao walifanikiwa kujiokoa na wengine hawakufanikiwa.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni zilionesha mtafaruku na hamaki za watu wakijaribu kujiokoa baada ya kutumbukia mtoni huku wengine wakikwama katika kingo za daraja hilo.
Juhudi za uokoaji zimekuwa zikifanyika usiku kucha lakini bado chanzo cha kuvujika daraja hilo hakijajulikana huku mamlaka ya eneo hilo ikidai kuwa msongamano wa watu katika daraja hilo huwenda ukasababisha.
Imeandaliwa na Sanifa Khalifa kwa msaada wa mtandao