
MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ameibua tena bungeni sakata la Sh. trilioni 360 za malimbikizo ya kodi za makinikia na kutaka serikali iliambie Bunge ukweli.
Akichangia jana bungeni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mpina alisema maelezo yaliyotolewa kuhusu fedha hizo kwamba zimeshasamehewa zote huku ikidaiwa hazijasamehewa, yanapaswa kuwekwa sawa ili Bunge lipate hatima ya fedha hizo.
Alisema kodi hizo zilikuwa zimeshikiliwa na mamlaka za rufani za kikodi za TRAB na TRAT.
“Serikali ilituambia hapa Januari 2020 serikali ilifuta madai haya, lakini taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/20, inatambua serikali inadai Sh. trilioni 360 na ilipofikia taarifa ya CAG ya mwaka 2020/21 anasema inaonyesha kuwa kesi za makinikia zenye thamani ya Sh. trilioni 5.595 zimeamriwa na TRAB na TRAT na ilipoamriwa serikali iliagizwa kufanya majadiliano na kampuni zilizopaswa kulipa kodi hizo,” alisema.
Mpina alisema amefuatilia ripoti za viongozi ikiwamo vikao vyote vya Hayati Rais Dk. John Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan kama waliwahi kuzungumza kusamehe kodi hizo za Sh. trilioni 360.
“Hawajawahi kuzungumza fedha hizi zimefutwa, mahakama iliagiza kampuni za madini na serikali wajadiliane namna ya kulipa Sh. trilioni 5.595, sasa aliyeagiza kodi hizo zisamehewe ni nani? CAG alete taarifa juu ya jambo hili ili Watanzania wajue hitimisho na fedha zao.
“Nchi hii maskini haiwezi kuingia makubaliano ya kusamehe kodi kubwa hizo, halafu tukaendelea kutoza kodi ndogo ndogo kwa wananchi, tunaacha wafanyabiashara wakubwa kama hawa wanasamehewa na nani? Na tulishaeleza hizi kodi zilipatikanaje.
“Serikali itoe kauli kuhusu hili na CAG akachukue nyaraka zote kama Dk. Magufuli alisamehe hili deni au Rais Samia. Tuletewe hapa ili tufanye uamuzi kama Bunge,” alisema.
Kauli hiyo ilimwinua kwenye kiti Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Simbachawene, akimtaka Mpina kueleza vizuri kinachotokea kwenye rufani za kikodi kukiwa na mgogoro na kodi.
Simbachawene alisema kuna wanaodaiwa walishafunga kampuni na mazingira ya aina hiyo yalichangia wawekezaji kuondoka.
PAC NA MADUDU
Awali Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilibainisha ‘madudu’ ya upotevu wa fedha katika mashirika mbalimbali ya umma kwa mwaka 2020/21, ikiwamo Mamlaka ya Mapato (TRA) iliyoshindwa kukusanya mapato kwa asilimia 14 sawa na Sh. trilioni 2.8.
Kamati hiyo pia imebaini Shirika la Umeme (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Shirika la Madini (STAMICO) kwa mwaka huo yalikuwa na uwiano usio mzuri wa madeni kulinganisha na mtaji wa jumla.
Taasisi zingine zilizobainika kufanya vibaya ni pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), benki za TIB, TCB, Mfuko wa Jeshi la Polisi wa Tuzo na Tozo na Jeshi la Uhamiaji.
Akiwasilisha bungeni jana jijini Dodoma taarifa ya PAC, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga, alisema TRA ilifanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato kulinganisha na makadirio waliyojiwekea kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2021 na kwamba kulikuwa na nakisi ya ukusanyaji wa mapato ya Sh. trilioni 2.8 na imechangiwa na matatizo mbalimbali likiwamo ongezeko kidogo la makusanyo ya kodi.
Hasunga alisema kamati imetoa mapendekezo katika maeneo mahsusi ikiwamo kuishauri TRA kuboresha mifumo yake ya ukusanyaji wa kodi na serikali kuboresha shughuli za vyombo vinavyohusika na kushughulikia rufani za kodi (TRAT na TRAB).
Kamati hiyo pia imependekeza Msajili wa Hazina kuangalia namna bora ya kuongeza mtaji katika Mashirika ya kimkakati ya TANESCO, TPDC na STAMICO.
Kuhusu ukaguzi maalum Idara ya Uhamiaji (Viza na stika bandia), Hasunga alisema ulibaini wageni 33,558 waliwasili nchini kupitia KIA, lakini taarifa zao ambazo ni pamoja na fomu za kuingia nchini, stakabadhi za mapokezi ya fedha (ERV) na uwekaji fedha benki hazikupatikana kwa ajili ya uhakiki.
Kwa sababu hiyo, ukaguzi haukuweza kuthibitisha kiasi cha mapato ambacho serikali ilipaswa kupata kutoka kwa wageni hao na kupendekeza watumishi wa idara ya uhamiaji 32 wachukuliwe hatua.
Hasunga pia alisema kamati imebaini mifuko ya PSSSF na NSSF haijapata faida katika miradi iliyowekeza mabilioni ya shilingi kutokana na kutokuwa na mikakati madhubuti ya masoko na mauzo.