
KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta amebainisha kuwa kwa sasa Arsenal ipo kwenye mbio za kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu ya Nchini Uingereza baada ya kuichapa Chelsea kwa bao 1-0.
Arsenal ilipata ushindi huo wa bao 1-0 kupitia kwa mlinzi wake wa kati Gabriel kufuatia mpira wa kona uliopigwa na winga wa timu hiyo Bukayo Saka.

Akiongea na waandishi wa Habari Arteta amenukuliwa akisema:
“Angalia namna ambavyo Manchester City yenye wachezaji bora duniani pamoja na kocha bora duniani kitu walichokifanya kwa miaka 6 iliyopita, kiukweli tunagombania ubingwa lakini lazima tuwaheshimu Manchester City kwa namna walivyokuwa na mwendelezo mzuri kwa kipindi kirefu, ni kweli leo tupo kwenye nafasi nzuri lakini kesho ni ngumu.”
Kwa sasa Arsenal ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza ikiwa na jumla ya alama 34 baada ya kucheza michezo 13 huku ikifuatiwa na Manchester City katika nafasi ya pili ikiwa na jumla ya alama 32 nayo ikiwa tayari imecheza michezo 13.