×

TPSF Yatangaza Siku ya Sekta Binafsi Tanzania, Yazindua Nembo Yake Rasmi

Bi Angelina Ngalula.

 

 

Alhamisi, Novemba 10, 2022, Dar es Salaam: TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania inatarajia kuadhimisha Siku ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSD22) ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Desemba 2022. Tukio hilo litafanyika kwenye ukumbi wa The Super dome Arena, Masaki Dar es Salaam Tanzania.

Sehemu ya wadau kwenye uzinduzi huo.

 

 

TPSD22 imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta binafsi na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kuenzi na kutambua mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi. Zaidi ya wajumbe 1,000 ambao ni viongozi wa kisekta, wakurugenzi watendaji na maafisa waandamizi wa serikali watakusanyika kujadili dhima kuu ya “Kuimarisha Ushindani wa Sekta Binafsi”.

Uzinduzi huo ulivyofanyika.

 

 

“Lengo la tukio hili ni kutathmini mafanikio ya sekta binafsi katika kipindi cha 2021-2022, huku tukiangazia mazingira bora ya biashara na uwekezaji ambayo yamechochea ukuaji wa uchumi chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita,” alisema, Bi Angelina Ngalula.

 

 

Ongezeko la biashara na majirani zetu   Kenya kwa asilimia 95 kumechangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Mafanikio mengine muhimu ya sekta binafsi ni pamoja na ukuaji wa shughuli za uwekezaji, upanukaji wa wigo wa ajira, masuala ya kodi, na bidhaa za Tanzania kufikia masoko mapya.

 

Ngalula alibainisha kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Sekta Binafsi yatatumika kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo. “Tunatakiwa kuueleza ulimwengu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania,” Ngalula alisisitiza. Mwenyekiti wa TPSF alisema, kilimo ni sekta yenye kuleta faida kubwa kwa watu wenye nia ya kuwekeza.

 

“Hivi karibuni tumesaini mikataba muhimu ambayo imepelekea mazao kutoka Tanzania kuuzwa nchi za nje. Kwa mfano, China imeagiza zaidi ya tani 40,000 za maparachichi kutoka Tanzania.  Tumeshuhudia makubaliano kama haya yakifanyika baina yetu na Afrika Kusini na India.”

 

Kupitia diplomasia ya uchumi, Ngalula alisema, fursa za uwekezaji kwenye sekta ya madini zinatangazwa nje ya nchi na matokeo yake sasa yanaonekana. Mwaka 2021, serikali ilisaini mikataba mine na makampuni ya uchimbaji madini yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 735, mikataba hii ni yenye thamani kubwa zaidi nchini Tanzania.

 

Kwa mujibu wa mwenyekitiwa TPSF, kiwango cha ukuaji wa uchumi baada ya janga la UVIKO-19 kinatakiwa kuendelea, akisema kuwa hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 5.1, Sekta binafsi imekuwa sehemu ya kutoa suluhisho kwa changamoto za uchumi kupitia biashara ndogo na za kati ambazo ni chanzo cha kipato kwa familia na uchumi wa taifa.

 

“Familia nyingi Tanzania zinategemea biashara ndogo na za kati, kwa mujibu wa Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA) takribani asilimia 35 ya pato la taifa linatokana na kundi hili. Maongezi yetu ya Disemba yatajikita katika nafasi ya sekta binafsi kwenye kuisaidia nchi kufikia dira yake ya maendeleo,” Ngalula alifafanua.

 

Aidha, TPSF itazindua makongamano ya kikanda ya wauzaji na wanunuzi yaani ‘Zonal Buyer-Seller Forums.’  Makongamano haya yanalenga kukuza biashara na uwekezaji kuanzia kwenye ngazi za mikoa na wilaya.  Lengo letu ni kuongeza mauzo baina ya biashara katika kanda zote nchini Tanzania.

 

Kwa kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya ushauri, Epvate& Fortune International Consulting (EFIC), TPSF pia itatoa tuzo na kutambua makampuni na mashirika binafsi (PSOs) ambayo yameonyesha utendaji wa kipekee ndani ya mwaka mzima.

 

“Tutatoa zawadi kwenye vipengele vifuatavyo: (i) vyama vya biashara vyenye michango maalum kwenye sekta, (ii) kampuni yenye shughuli bora zaidi za kusaidia jamii (CSR), (iii) kampuni inayochipukia (Startup) yenye ubunifu zaidi, (iv) kampuni bora katika utunzaji endelevu wa mazingira, na (v) taasisi za serikali zinazowezesha biashara, ”Ngalula alimaliza kusema.

 

KUHUSU TPSF

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ni sauti ya sekta binafsi nchini Tanzania. TPSF inawakilisha zaidi ya biashara milioni nne na ina zaidi ya wanachama 375 wa moja kwa moja.

Tovuti: www.tpsftz.org

Twitter @tpsftz

Instagram: @tpsf_tanzania

LinkedIn: Tanzania Private Sector Foundation

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na: Jackline Isaack, Afisa Mawasiliano na Mahusiano na Umma (0717577217)

Leave a Comment