
Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo amesema kuwa mataifa ya Afrika lazima yajiondoe kwenye utaratibu wa kuomba nchi za Magharibi ili kupata heshima ya kimataifa na kubadili mitazamo duni kuhusu bara hilo.
“Tukiacha kuwa ombaomba na kutumia pesa za Kiafrika ndani ya bara hili, Afrika haitakuwa na haja ya kuomba heshima kutoka kwa mtu yeyote, tutapata heshima tunayostahili. Tukifanikisha hilo basi, heshima itafuata,” Bw Akufo -Ado alisema. Hayo ameyasema wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Marekani na Afrika unaofanyika mjini Washington DC.
Bw Akufo-Addo alihimiza mshikamano zaidi miongoni mwa Waafrika ili kushughulikia malengo ya pamoja.
“Waafrika wanastahimili zaidi nje ya bara kuliko ndani. Lazima tukumbuke kwamba kwa ulimwengu wa nje, hakuna kitu kama Nigeria, Ghana au Kenya, sisi ni Waafrika tu. Hatima yetu inategemea kila mmoja,” alisema.
Rais alisema kuwa bara hilo lilikuwa na ujuzi na wafanyakazi lakini lilihitaji utashi wa kisiasa wa kufanya “Afrika ifanye kazi”. Matamshi ya Bw Akufo-Addo yalikuja siku ambayo Shirika la Fedha la Kimataifa kukubali kuipa Ghana mkopo wa $3bilioni (£2.4bn) ili kupunguza mtikisiko wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Makumi ya viongozi wa Afrika wako mjini Washington kujadili ushirikiano na Marekani huku kukiwa na ongezeko la ushawishi wa China na Urusi katika bara hilo.