
Dubai imefutilia mbali ushuru wake wa 30% wa pombe katika jitihada za kuimarisha utalii.
Pia itaacha kutoza leseni za pombe za kibinafsi – kitu ambacho mtu yeyote anayenuia kunywa anahitaji kubeba.
Dubai imekuwa ikilegeza sheria kwa muda, ikiruhusu uuzaji wa pombe mchana wakati wa Ramadhani na kuidhinisha mauzo ya pombe majumbani wakati wa janga la Corona.
Hatua hii ya hivi punde inadhaniwa kuwa ni jaribio la kulifanya jiji kuvutia wageni Zaidi licha ya ushindani kutoka kwa majirani.
Kampuni mbili zinazosambaza pombe huko Dubai, Maritime na Mercantile International (MMI), na African & Eastern, zilisema zitaakisi kupunguzwa kwa ushuru kwa watumiaji.
“Kanuni hizi zilizosasishwa hivi majuzi ni muhimu kuendelea kuhakikisha ununuzi na unywaji salama na unaowajibika wa vileo huko Dubai na UAE.”
Haijabainika iwapo hatua hiyo iliyoanza kutekelezwa Jumapili, itakuwa ya kudumu. Gazeti la Financial Times
lilielezea hatua hiyo kama jaribio la mwaka mmoja, likinukuu “watendaji wa sekta walio na ufahamu kuhusu uamuzi huo”.
Wakazi kutoka nje huzidi idadi ya raia kwa tisa kwa mmoja huko Dubai, unaojulikana kama “mji mkuu wa karamu” wa Ghuba, na wakaazi kwa kawaida huendesha gari hadi Umm al-Quwain na falme zingine kununua pombe kwa wingi.
Dubai kihistoria imeweza kuvutia watalii zaidi na wafanyikazi matajiri wa kigeni kuliko majirani zake, kwa sehemu kwa sababu ya uvumilivu wake wa maisha ya huria zaidi.
Lakini sasa inakabiliwa na ushindani unaoongezeka kutoka kwa wapinzani wanaoendeleza sekta zao za hoteli ,burudani na fedha.
Wasio Waislamu nchini Dubai lazima wawe na umri wa angalau miaka 21 ili kunywa pombe, na kubeba leseni ya pombe – kadi ya plastiki iliyotolewa na polisi.
Ingawa baa na vilabu vya usiku ni nadra sana kuviomba vibali hivyo wale wanaokunywa pombe bila vibali wanaweza kutozwa faini au kukamatwa.