
WANAFUNZI 32 wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Mkomo, Kata ya Chawi Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara, wamenusurika kifo baada ya kula matunda ya porini yanayodhaniwa kuwa na sumu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bakari Likuani amenukuliwa akieleza kuwa tukio hilo limetokea wakati wa mapumziko ambapo watoto hao walitoka darasani baada ya kengele ya uji kugongwa ambapo wakiwa nje, ndipo waliposhambulia matunda hayo.
Likuani ameongeza kuwa takribani nusu saa baada ya kula matunda hayo, mtoto wa kwanza alianza kutapika ambapo mwalimu wake alihisi anaumwa hivyo akamruhusu kurudi nyumbani lakini muda mfupi baadaye, watoto wote wa darasa hilo, nao walianza kutapika, jambo lililowalazimu kuwakimbiza hospitali.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Zahanati ya Chawi, Kandidusi Fussi amesema kuwa aliwapokea watoto 32 wenye umri kati ya miaka 5-6 wa darasa la awali kutoka Shule ya Msingi Mkomo wanaodaiwa kula matunda yenye sumu.
Ameeleza kuwa walifikishwa wakiwa na hali mbaya, wakiwa wamelegea na wakitapika ambapo waliwapa huduma ya kwanza ya kuwanyweshwa maziwa ambapo walitapika zaidi na baadaye, walipata nafuu na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.