
MANCHESTER City walirejea kileleni mwa Ligi Kuu England (EPL) kwa mara ya kwanza tangu Novemba walipowachapa viongozi wa ligi hiyo kwa muda mrefu, Arsenal mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Emirates, London usiku wa kuamkia jana.
City, walianza kuongeza nguvu kipindi cha pili katika mchezo mkubwa zaidi wa msimu huu kwao, huku Arsenal wakilipa gharama kubwa kwa makosa ya kibinafsi kutoka kwa wachezaji wao.
Pasi ya nyuma ya Takehiro Tomiyasu ilimruhusu Kevin de Bruyne kumalizia mpira uliopita juu ya kipa wa Arsenal, Aaron Ramsdale baada ya dakika 24 za kipindi cha kwanza, lakini Arsenal walikwenda mapumziko wakiwa na bao moja.
Dakika tatu kabla ya kipindi cha mapumziko, Bukayo Saka alifunga mkwaju wa penalti baada ya kipa wa City Ederson kumchezea vibaya Eddie Nketiah.
City, ambayo ilitengeneza nafasi cheche katika dakika za mwanzo, iliimarika baada ya mapumziko na kupata penalti, iliyokataliwa kwa madai ya kuotea kwa Erling Haaland.

Gabriel beki wa Arsenal, alipoteza mpira kizembe na kuwaruhusu Bernardo Silva na Haaland kumtengenezea Jack Grealish nafasi ya kufunga bao la pili kwa City dakika 72 kabla ya timu hiyo kupata bao la tatu kupitia kwa muuaji wao mwenye roho katili zaidi, Haaland.
KASI YA MAN CITY INASHTUA
City wamerejea kileleni mwa Ligi ya EPL, wakiwa na moto mkali kiasi cha kuanza kuonekana kama wanaweza kubeba taji tena msimu huu.
City walikosa ufasaha wao wa kawaida katika dakika 45 za kwanza na bila shaka Arsenal walistahili zaidi ya kipigo hiki kutokana na makosa waliyofanya.
Hata hivyo, mara tu ya kipindi cha pili City walikuja kuwa tishio la kutosha kuwaweka Arsenal mbali ya kupata alama tatu ambazo walikuwa wanazihitaji zaidi.
Lakini kwa bahati City waliweza kurejea kwenye nafasi ambayo wamekuwa wakikaa mara nyingi katika miaka ya hivi karibuni
ARSENAL BADO WAPO MBIO ZA UBINGWA
Kichapo hiki kitakuwa pigo chungu kwa Arsenal kama ilivyokuwa mbele ya mashabiki wao. Ingawa bado wanayo nafasi ya kurejea tena kileleni kwa kuwa tofauti yao na City ni mabao na vijana wa Mikel Arteta wana mchezo mmoja mkononi.
Ingawa, ukweli ni kwamba wamepoteza mara mbili mfululizo mbele ya City kwa kipindi kisichozidi wiki mbili. Walifungwa kwenye Kombe la FA na Everton kwenye ligi, walitoka sare ya kutatanisha dhidi ya Brentford kwenye ligi.
ARSENAL WANAPASWA KUWA JASIRI
Arsenal na Arteta hawapaswi kujidharau sana, ingawa ukubwa wa kushindwa hapa hauwezi kupuuzwa katika muktadha wa mbio za ubingwa.
The Gunners, kila mmoja ana imani nao, kazi itabaki kuwa kwao kutofanya makosa ya kizembe kama ambayo wamefanya mbele ya City. Ingawa sasa presha yao itakuwa juu zaidi.
Kwa kuwa hawajapata alama tatu kwenye mechi tatu mfululizo za EPL, hii siyo ishara njema kwa timu ambayo inakuwa inawania ubingwa.

RATIBA YA ARSENAL FEBRUARI
Februari 4—Everton 1-0 Arsenal
Februari 11—Arsenal 1-1 Brentford
Februari 15—Arsenal 1-3 Man City
Februari 18—Aston Villa vs Arsenal
Februari 25— Leicester vs Arsenal
RATIBA YA MAN CITY FEBRUARI
Februari 5—Tottenham 1-0 Man City
Februari 12—Man City 3-1 Aston Villa
Februari 15—Arsenal 1-3 Man City
Februari 18—Nottingham vs Man City
Februari 25—Bournemouth vs Man City
NAKALA NA Issa Liponda