
WAKATI Yanga ikiwa na kazi ya kusaka ushindi leo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe, wamewataja mastaa watakaomaliza kazi na kuwapa furaha Wananchi.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kuanzia saa 1:00 usiku ikiwa ni mchezo wa pili wa Kundi D.
Ikumbukwe kwamba, katika mchezo wa kwanza ugenini, ubao ulisoma US Monastir 2-0 Yanga, hivyo wachezaji wataingia wakiwa na hesabu za kutafuta ushindi kwenye ardhi ya Tanzania.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema wanatambua kazi itakuwa ngumu kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe, lakini wana wachezaji wenye uwezo wa kufunga.
“Ninaamini kwamba mnajua ndani ya Yanga yupo Fiston Mayele ambaye huyu ukimtaja unazungumzia mabao, mbali na huyo wapo wengine ikiwa ni pamoja na Aziz KI.
“Pia mpaka mabeki ndani ya kikosi chetu wanafunga na wanatimiza majukumu yao kwa umakini kama ilivyo kwa Dickson Job, Yannick Bangala, hivyo uwepo wao ni moja ya sababu kwetu kuamini tutapata matokeo mazuri.
“Mashabiki tunawaomba mjitokeze kwa wingi kutushangilia na uwepo wenu utatufanya tupate matokeo bora, kila kitu kinawezekana,” alisema Kamwe.
STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA