
UONGOZI wa Simba, umetoa tamko kwamba, wapinzani wao wa kimataifa ambao wana zamu ya kushuka Uwanja wa Mkapa jijini Dar, watakutana na pumzi ya moto ambayo itakuwa simulizi kwa wengine.
Mchezo wa kwanza Simba kutupa kete yake Uwanja wa Mkapa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi msimu huu, ilikutana na kitu kizito baada ya kuchapwa mabao 0-3 dhidi ya Raja Casablanca.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema: “Raja Casablanca walikuwa bora kwa siku hiyo, wakapata ushindi, lakini Horoya na Vipers lazima watakutana na pumzi ya moto ili wakawasimulie wengine.

“Haina maana kufungwa na Raja Casablanca watakaokuja wataendelea kupata ushindi, hilo wasahau, lazima tuwaambie kwamba hii ni Dar na pale ni Benjamini Mkapa, hivyo lazima tuwapalekee pumzi ya moto.
“Mashabiki waliumia na maumivu haya yapo kwetu, lakini huo mchezo umeshapita na sisi tumechagua kusonga mbele kwa kuwa lazima mapambano yaendelee na tupo tayari, wageni wakaribie, watapata kile kinachowastahili kabisa.
Simba ambayo jana ilikuwa Uganda kucheza dhidi ya Vipers, katika Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika, imesaliwa na mechi tatu, mbili nyumbani dhidi ya Vipers (Machi 7) na Horoya (Machi 17 au 18), kisha ugenini dhidi ya Raja Casablanca (Machi 31 au Aprili 1).