×

Watanzania Wang’ara Kilimanjaro International Marathon

Mshindi wa Mbio za Km 42, Sarah Ramadhani wa hapa Tanzania hivi ndivyo alivyomaliza mbio zake.

KILIMANJARO 26 FEBRUARI 2023: Wanariadha wa kitanzania wameng’ara katika mbio za 21 za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon, baada ya kufanya vizuri katika mbio za Km42 na 21.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika jana, Moshi, mkoani Kilimanjaro, Aloyce Simbu kutoka Tanzania alishika nafasi ya pili katika mbio za Kilimanjaro Premium Lager kilomita 42 wanaume baada ya kukimbia kwa saa 2:18:29 akiwa ametanguliwa na Mkenya Kenneth Kiprop Omulo alieshika nafasi ya kwanza baada ya kukimbia kwa saa 2:18:05.

Mshindi wa Km 21, Emmanuel Giniki wa Tanzania alivyomaliza mbio hizo.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Abraham Kosgei kutoka Kenya aliekimbiakwa saa 2:19:30, ambapo washindi wengine na nafasi walizoshika zikiwa kwenye mabano ni Paul Damian, Tanzania (4), Rashid Muna, Tanzania (5), Amos Kirwa Tanzania, (6), Benard Kigen, Tanzania (7), Khamis Athuman, Tanzania (8), Benson Kosgei, Kenya (9) na Marcel Sarwat wa Tanzania (10).

Katika upande wa wanawake, wanariadha wa Tanzania walishika nafasi tatu za kwanza ambapo Sarah Ramadhan alishika nafasi ya kwanza baada ya kukimbia kwa saa 3:02:36 na kumshinda Neema Sanka alieshika nafasi ya pili kwa kukimbia kwa saa 3:20:05. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mtanzania mwingine Visa Mhalwa aliekibmia kwa saa 3:25:14.

Magdalena Shauri wa Tanzania akimaliza mbio hizo kwa ushindi.

Washindi wengine kwa mujibu wa kumi bora kwenye kitengo hiki ni pamoja na Jane Mathenge wa Kenya, (4), Rebecca Nakuwa, Tanzania (5), Immaculate Wanjiku, Kenya (6), Mary Atto, Kenya (7), Claire Baker, Kenya (8), Justina Kilumelume, Zambia (9) na Patricia Mabena, Tanzania (10).

Katika mbio za kilomita 21 zinazodhaminiwa na Tigo, mshindi kwa upande wa wanaume Watanzania wakiongozwa na Emmanuel Giniki walishika nafasi nne za kwanza ambapo Giniki aligona muda wa saa 1:00:36. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Josephat Gisemo aliekimbia kwa muda wa 1:05:12 akifuatiwa kwa Karibu na Decta Teziforce aliekimbia kwa muda wa saa 1:05:43 na kushika nafasi ya tatu.

Mtanzania Aloyce Simbu akivishwa medali baada ya kumaliza mbio za km 42 akiwa nafasi ya pili.

Katika hotuba yake baada ya mashindano hayo Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa aliwapongeza washindi wa mbio hizo ambapo alisema mafanikio yao yameakisi matayarisho mazuri waliyoyafanya kabla ya kushiriki kwao.

“Ushindi wenu ni chachu kwa wengine kujiandaa vyema mwakani ili wafanye vizuri na kwenu itakuwa unawapa moyo wa kujituma Zaidi ili kulinda mafanikio mliyoapata”, alisema.

Mgeni rasmi katika mbio hizo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja naye hivi ndivyo alivyomaliza mbio za km 5.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mary Masanja, Mchengerwa alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na waratibu na wadau wengine wa mbio hizo kutokana na umuhimu wake kwa Taifa.

“Mashindano haya ni muhimu kwa nchi yetu kutokana na ukweli ya kuwa mbali na kukuza kiwango cha michezo nchini pia yanachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii hapa nchini”, alisema.

“Kutokana na mashindano haya kushirikisha na kuleta watu wengine kutoka mataifa zaidi ya 50 duniani kote, pia yanawezesha kutangazwa kwa vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro pamoja na kukuza utalii wa Zanzibar kwa kutangaza vivutio vilivyoko kisiwani humo”, alisema.

Mshindi wa kwanza Wanawake, mbio ndefu za km 42, Sarah Ramadhani (katikati) akionesha furaha baada ya kukabidhiwa mfano wa hundi ya fedha alizojishindia.

Aidha Waziri Mchengerwa alitoa shukrani kwa waandaaji na wadhamini wa mbio o maarufu Barani Afrika kwa namna tuwalivyoshirikiana nae wakati akiwa Waziri wa Utamaduni na Michezo, ambapo alisema kuwa Serikali inaendelea kuona umuhimu wa tukio hili la kipekee katika sekta ya utalii ambayo ameanza kuitumikia hizi karibuni.

“Hongereni sana kwani nimefahamishwa kuwa hii ni mbio ya 21 tangu kuanzishwa kwa mbio hizi maarufu; sisi kama serikali tunajivunia tukio hili ambalo linapeperusha bendera ya Taifa letu sio kimichezo tu, bali hata katika sekta ya utalii, kwani sasa hivi kila mtu duniani anazungumzia sports tourism na Kilimanjaro International Marathon kama mfano bora wa tukio la kimataifa linalotambulika, kukumbukwa na kusubiriwa kila mwaka”.

Mshindi wa mbio za km 21 Wanawake Magdalena Shauri akipewa mfano wa hundi ya fedha alizojishindia baada ya kuibuka mshindi wa kwanza.

Aidha Waziri Mchengerwa aliwapongeza washindi wote katika mbio zote za Kilimanjaro Premium Lager km 42, Tigo Km21 na Grand Malt Km 5.

Aidha aliwapongeza wandaaji wa mashindano hayo kwa kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa ya kuyapandisha hadhi mashindano hayo ambayo kwa sasa yanajulikana kama Kilimanjaro Premium Lager International Marathon na hivyo kuzifanya mbio hizo kongwe kuliko zote hapa nchini ziendelee kuwa maarufu duniani kote na kuhusisha zaidi ya washiriki 12,000 kutoka mataifa zaidi ya 50.

Pia aliwapongeza wandaaji wa mbio hizo kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na chama cha riadha duniani (World Athletics) na kila cha hapa nchini (RT) kwa michango yao iliyochangia Kilimanjaro Marathon iendelee kuwa maarufu.

Waziri Mchengerwa pia aliwapongeza wadhamini wote wa mbio hizo wakiongozwa na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini uliotukuka wa miaka 21.

Aidha aliwapongeza wadhamini wengine ambao alisema ni pamoja na kampuni ya Tigo inayodhamini mbio za Km 21 na Grand Malt mbio za Km 5 maarufu kama Fun Run pamoja na wadhamini wengine ambao ni TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies  na watoa huduma rasmi wakimemo Surveyed Plots Company Limited (SPC), GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel  na CMC Automobiles na Salsalinero.

Aidha aliwapongeza wadau wengine ambao alisema ni pamoja na Chama Cha Riadha Tanzania, Baraza la Michezo Tanzania, Kamati ya Olympiki, Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU), jogging clubs mbalimbali, Jeshi la Polisi, waratibu wa ndani waandaji Kilimanjaro Marathon Company Ltd, waratibu Executive Solutions na waadishi wa habari.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TBL ambao ni wadhamini wakuu kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Jose Moran, alisema kampuni hiyo inafurahi kuwa sehemu ya tukio hili kubwa la kimtaifa ambalo limekuwa na mafanikio makubwa kwa miaka mingi.

“Tumekuwa wadhamini wakuu tangu mwanzo wa mashindano haya mwaka wa 2003 na kwa pamoja tumepiga hatua kubwa hadi leo tunapoadhimisha msimu wa 21 wa mafanikio makubwa”, alisema.

“Imekuwa safari ya kusisimua kwani hii sasa ndiyo mashindano makubwa zaidi ya riadha katika ukanda mzima wa Afrika kwani yanaleta kwa pamoja zaidi ya wakimbiaji 12,000 kutoka mataifa zaidi ya 55; hay ani mafanikio makubwa haswa ikizingatiwa tulianza na washiriki chini ya 750 tu miaka 20 iliyopita”, alisema na kuongeza tayari tukio hili limewavutia zaidi ya washiriki 160,000 kwa miaka 21 iliyopita haya ni maajabu.

Kwa upande Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tigo ambao ni wadhamini wa kilomita 21 ya mbio hizo, Innocent Rwetaburwa alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa mashindano hayo kutokana na umuhimu wake kwa Taifa katika kukuza michezo na uchumi wa Taifa.

“Tumekuwa wadhamini wa Tigo Kili Half Marathon kwa miaka nane sasa; udhamini huu ni sehemu ya mikakati yetu katika kuungana na wandaaji wa mbio hizi katika kukuza vipaji, sekta ya michezo na sekta ya utalii kupitia dhana ya sports tourism”, alisema.

Katika mashindano hayo, washindi wa Kitanzania walioshika nafasi ya kwanza miongoni mwa washiriki Wakitanzania katika vipengele vyote vya wanaume na wanawake vya mbio za kilomita 42, walizawadiwa na wadhamini wakuu mbio hizo, Kilimanjaro Lager zawadi ya motisha ya shilingi milioni 1.5 kila mmoja.

Waliobahatika kupata motisha hizo ni Aloyce Simbu ambaye kwa kushika nafasi ya pili kwa upande wa wanaume kilomita 42, alikuwa ndiye mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na kujinyakulia jumla ya shilingi milioni 3.6 na Sarah Ramadhan ambaye ndiye alikuwa mshindi kwa upande wa wanawake mbio za kilomita 42 ambapo kwa mafanikio hayo amejinyakulia jumla ya shilingi milioni 5.7.

Leave a Comment