Waziri wa maji, Mhe Jumaa Aweso (Mb) amewataka watendaji kutozoea shida za Wananchi na kuhimiza uwajibikaji utakaoleta tija kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza Wizara kujipanga upya na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kushughulikia changamoto za wananchi katika dhana ya kupata huduma ya Maji.

Waziri Aweso ameyasema hayo wakati alipofanya kikao cha dharula cha Menejimenti ya Wizara pamoja na kuwaungamisha moja kwa moja kwa njia ya mtandao watendaji wote wa Sekta ya Maji mikoani ikiwa ni pamoja na Mameneja wa Maji vijijini mikoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji, Wakurugenzi wa Mabonde na Ubora wa Maji na Chuo cha Maji akiwakaribisha watendaji walioteuliwa na Mhe Rais hivi karibuni ambao ni Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Amesema wizara ya Maji inakamia kutekeleza ilani ya Chama Tawala ya upatikanaji wa huduma ya maji ya asilimia 95 mjini na asilimia 85 vijijini ifikapo 2025.

“Serikali yetu chini ya uongozi wa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan inadhamira ya dhati ya kuwaondolea wananchi changamoto ya maji, hivyo kila mtendaji katika sekta ya maji awajibike vyema katika kusimamia jambo hili lenye maslai mapana ya nchi yetu. Tuache mazoea kwa shida za wananchi ambao tumepata dhamana ya kuwahudumi.” Aliongeza.

Kwa upande wake, katibu mkuu wizara ya maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amewakumbusha watumishi kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa katika kutoa huduma na kuongeza mahusiano baina ya watendaji na wananchi ili kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali.