×

Vigogo Simba wamfungia kazi Nabi Waandaa Bonasi ya Sh 300Mil kwa Wachezaji

Kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Simba  wakijadili mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya klabu hiyo. Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Salim Muhene Aprili 12, 2023.

MABOSI wa Simba wameamua kuifungia kazi Yanga inayonolewa na Kocha, Nasreddine Nabi kwani wamesema hawataki chochote zaidi ya ushindi katika Kariakoo Dabi, ambapo tayari wameandaa bonasi ya kutosha ya zaidi ya Sh 300Mil kwa wachezaji ili kufanikisha ushindi.

Kariakoo Dabi hiyo itakuwa ya raundi ya pili katika Ligi Kuu Bara, itakayochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Simba wataingia wakiwa na hasira ya kufungwa mara mbili mfululizo walizokutana katika Ngao ya Jamii msimu huu na uliopita.

Simba mara zote hizo, wamefungwa na mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele, msimu uliopita bao 1-0 na huu 2-1.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, mabosi hao wa Simba kitu pekee ambacho wanakitaka katika msimu huu ni kuifunga Yanga, hiyo ni baada ya kushindwa kuifunga kwa misimu miwili.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mabosi hao wa Simba, wameweka nguvu hizo za kuwafunga Yanga kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wao.

Kocha, Nasreddine Nabi.

Aliongeza kuwa, mabosi hao wanaamini ushindi watakaoupata katika dabi hiyo, itawasahaulisha machungu ya kuukosa ubingwa ambao asilimia kubwa inaonekana Yanga inakwenda kuubeba.

“Viongozi wetu wanaitaka kwelikweli Kariakoo Dabi, wakiamini ni sehemu ya kuwapooza machungu mashabiki wao kwa kuukosa ubingwa wa ligi kwa misimu mwili ambayo yote imekwenda Yanga.

“Hivyo presha ya kupoteza ubingwa ipotee kwa mashabiki, ni lazima tuwafunge Yanga na hilo linawezekana kwetu, kwani fungu kubwa la kutosha la bonasi limeandaliwa ili kumfunga mtani wetu.

“Ni zaidi ya Sh 300Mil imetengwa na viongozi hao ili kufanikisha malengo, ahadi hiyo ya bonasi watatangaziwa siku ya Jumamosi usiku mara baadaya viongozi kula chakula cha jioni pamoja na wachezaji kambini,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akithibitisha hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Niseme kuwa tunauhitaji ushindi mkubwa katika dabi hii, hivyo ni lazima tuwafunge Yanga.”

“Binafsi tangu nimeingia Simba nikiwa kama kiongozi, sijawahi kushinda dabi yoyote, hivyo hii ni lazima tushinde ili na mimi niandike historia ya kuwafunga Yanga nikiwa kiongozi,” alisema Ally.

STORI NA WILBERT MOLANDI

“DAKTARI HARUHUSI KUUZA DAWA LAKINI MMASAI ANAKIBALI” – MBUNGE KISHIMBA ACHARUKA…

Leave a Comment