
SAA 11:00 jioni ya leo, sehemu kubwa ya Bara la Afrika itasimama kwa dakika tisini kushuhudia mchezo mkali wa Dabi ya Kariakoo unaotarajiwa kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hizo zinaingia katika mchezo huu zikiwa na kumbukumbu nzuri ya matokeo ya sare ya bao 1-1 mzunguko wa kwanza ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 23, 2022.
Tambo zimekuwa nyingi kwenye vijiwe vya soka mitaani ambapo kila upande umetamba kuibuka na ushindi katika shoo kali inayotarajiwa kushuhudiwa.

Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amesema: “Lengo letu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi na kucheza vizuri, nawajua vizuri wapinzani wetu Yanga, tunawaheshimu lakini tumejipanga. Mpira kwangu ni sanaa, napenda wachezaji wacheze na kuwafurahisha mashabiki.”
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema: “Tumejiandaa vizuri na kwa utulivu mkubwa, tunajua kesho (leo) tunakwenda kwenye moja kati ya michezo mikubwa Afrika na siyo kila mara tunacheza mechi inakuwa na mashabiki zaidi ya elfu hamsini, ni lazima tuwatendee haki na tumejiandaa vizuri kwa hilo.
“Kitu kizuri ni kwamba hatuna majeruhi zaidi ya Aboutwalib Mshery ambaye ni majeruhi wa muda mrefu, wachezaji wengine wote wapo salama.”

Spoti Xtra, linakuletea wachezaji wanaotarajiwa kuanza katika timu hizo kulingana na hali ilivyo.
SIMBA
KIPA: Aishi Manula, amewaondoa hofu Simba baada ya kuthibisha kupona jeraha la bega, msimu huu amefanikiwa kucheza mechi 23 kwa dakika 2,115, karuhusu mabao 13 akiwa na clean sheet 12
WALINZI: Israel Mwenda, anatarajiwa kuanza kufuatia majeraha ya Shomari Kapombe, msimu huu Mwenda amecheza mechi nne akitumika kwa dakika 292. Mohamed Hussein ameichezea Simba mechi 23 kwa dakika 2,138, ana pasi tano za mabao. Joash Onyango amesepa na dakika 1,469 kwenye mechi 19. Henock Inonga amecheza mechi 19, kasepa na dakika 1,524, katupia mabao mawili.
VIUNGO WA ULINZI: Mzamiru Yassin, amecheza mechi 23, katoa pasi tano za mabao na amefunga mabao mawili akiwa ameyeyusha dakika 1,776. Sadio Kanoute ametumika kwa dakika 1,348 akiwa amecheza mechi 18.
VIUNGO WASHAMBULIAJI: Clatous Chama mpaka sasa ndiye kinara wa pasi za mabao akiwa nazo 14, ametupia mabao matatu akiwa ametumia dakika 1,735 kwenye mechi 20. Pape Sakho amecheza mechi 21, kasepa na dakika 1,498, kafunga mabao saba, ana pasi moja ya bao. Saidi Ntibazonkiza amecheza mechi sita kwa dakika 536, kafunga mabao 6 akiwa ndani ya Simba, mabao manne akiwa Geita Gold. Jumla anayo 10.
MSHAMBULIAJI: Jean Baleke ambaye ametupia mabao 7 akiwa amesepa na dakika 367 kwenye mechi 4, hii ni dabi yake ya kwanza tangu atue Simba.
YANGA SC
KIPA: DJIGUI Diarra, amecheza mechi 22 kwa dakika 1,947, kafungwa mabao 10 akiwa na clean sheet 15.
WALINZI: Djuma Shabani amecheza mechi 15 kwa dakika1,036, ana bao moja na pasi mbili za mabao. Dickosn Job kasepa na dakika 1,755 kwenye mechi 20, ana bao moja. Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kacheza mechi 9, kasepa na dakika 626. Joyce Lomalisa mechi zake 16, ametumia dakika 1285, ametoa asisti tatu.
VIUNGO WA ULINZI: Yannick Bangala, amecheza mechi 16 kwa dakika 1,373, kafunga mabao mawili. Aucho Khalid amecheza mechi 19 na kusepa na dakika 1,475, ana pasi mbili za mabao.
VIUNGO WASHAMBULIAJI: Aziz Ki amecheza mechi 20, katupia mabao nane na pasi nne za mabao kwa dakika 1,279 alizocheza. Jesus Moloko, amecheza mechi 20 kwa dakika 1257, amefunga mabao mawili, ana pasi nne za mabao.
WASHAMBULIAJI: Fiston Mayele, amefunga mabao 16 na asisti moja. Kennedy Musonda, amecheza mechi tano, ana bao moja akiwa ameyeyusha dakika 268, hii ni dabi yake ya kwanza tangu atue Yanga.
STORI NA JOEL THOMAS NA LUNYAMADZO MLYUKA