×

Nabi Afanya Kikao Kizito na Wachezaji Wake Atoa Onyo Kisa Rivers United

Nasreddine Nabi.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, fasta amefanya kikao na wachezaji wake akiwataka wasibweteke na ushindi wa ugenini dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.

Yanga juzi ilipata ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Rivers United katika mchezo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Nigeria.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla atafuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi amewataka wachezaji wake kutobweteka na ushindi wa ugenini, hivyo wakumbuke wana kibarua kigumu katika mchezo wa marudiano huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa kuwapa sapoti.

Nabi alisema kuwa Rivers United sio timu dhaifu, kwani wana uwezo wa kupambana na kupata matokeo mazuri ugenini, hivyo wachezaji wake wana kibarua kigumu cha kupambana katika dakika zingine 90 kwenye Uwanja wa Mkapa.

“Hatujaja hapa Nigeria kujifurahisha, nazifahamu timu za Nigeria, kupata matokeo Nigeria ni vigumu sana, lakini tupo siriazi na mashindano haya. Nimekuwa nikiwaambia wachezaji wangu wajitahidi kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya kuwaza matokeo ya uwanja wa nyumbani, ndicho hicho nilichokifanya.

“Rivers ni timu nzuri, msimu wa 2021/22 walituondoa katika hatua za awali, kulikuwa na sababu nyingi lakini zaidi timu yetu haikuwa kwenye ubora tuliokuwa nao hivi sasa, kwani kikosi chetu kipo imara na tupo tayari kupambana.

“Uzuri ni kwamba Afrika tunajuana, mechi hii haijaisha, bado kuna mechi nyingine ya marudiano kwa Mkapa baada ya siku saba, kikao changu cha kwanza nilichokaa na wachezaji wangu kilikuwa cha msisitizo juu ya mchezo wa marudiano ambao hatutakiwi kuingia uwanjani tukiwa tunajiamini kuwa tumemaliza kazi.

“Nawaheshimu Rivers, kocha na wachezaji wao wote ni wazuri, lakini sisi tuna malengo ya kufika mbali zaidi kwenye mashindano haya,” alisema Nabi.

STORI NA WILBERT MOLANDI, SPOTI XTRA

DIAMOND na SHILOLE WAPATA UTEUZI, RAIS SAMIA AWATEUA KUWA WAJUMBE wa BARAZA la KUPAMBANA na MALARIA

Leave a Comment