
UONGOZI wa Simba umetuma ujumbe mzito kwa wapinzani wao Wydad Athletic Club kutoka mji wa Casablanca nchini Morocco kuwa wanakwenda kuwashangaza mbele ya mashabiki wao ‘vichaa’.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ambaye aliweka wazi kuwa Uwanja wa Mohamed V wanaufahamu na nyavu za uwanja huo zinamfahamu Jean Baleke hivyo wakae vizuri kuna jambo lao wanalitaka kwenye uwanja huo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Ahmed alisema, sababu ya Simba kuondoka mapema kwenda Morocco ni sehemu moja ya ujumbe kwa Wydad wajue kuwa wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo kuliko kitu kingine chochote na kwenye akili ya kila mchezaji ni kwenda nusu fainali tu.

“Ujumbe uwafikie Wydad Casablanca, sifa ya mashabiki wao tunayo na kwa bahati nzuri walituonesha hapa kwa Mkapa na tunajua ukichaa wao. Wachezaji wetu wamesema wanakwenda kuishangaza Afrika.
“Jean Baleke anaujua ule uwanja vizuri sana na ana bao lake pale Mohamed V, amesema anataka kuwafunga tena. Simba inataka nusu fainali na hakuna kitu kingine ambacho tunakiwaza kwa sasa,” alisema.
Simba waliondoka nchini kwa mafungu kuanzia Jumatatu na jana Jumanne kwenda Morocco kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano utakaochezwa mwishoni keshokutwa Ijumaa saa 4:00 usiku kwa saa za Bongo.
Stori: Issa Liponda