×

Bocco: Tumeumizwa Lakini Tumejifunza Baada ya Kupoteza nchini Morocco

BAADA ya kutua nchini jana Jumapili wakitokea Morocco walipoondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Bocco amekiri ni kweli wameumizwa na matokeo hayo lakini kuna vitu vingi wamejifunza ambavyo anaamini vitawasaidia kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo.

Simba usiku wa Ijumaa wakicheza kwenye Uwanja wa Mohammed V nchini Morocco walitolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya wenyeji wao, Wydad Casablanca katika mchezo wa robo fainali ya pili ya mashindano hayo.

Msafara wa Simba ulirejea nchini jana Jumapili asubuhi tayari kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya michezo yao iliyosalia ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Bocco alisema: “Kama wachezaji tumeumizwa na matokeo ambayo tumeyapata Morocco kwa kuwa malengo yetu yalikuwa kuhakikisha tunacheza nusu fainali ya mashindano haya, lakini kwenye mpira matokeo kama haya hutokea na hatuwezi kubadilisha kilichotokea zaidi sana tunapaswa kupambana na ratiba ya mashindano iliyo mbele yetu.

“Licha ya kwamba tumetolewa, lakini kuna vitu ambavyo tumejifunza na kwa mtu anayejua mpira anaona kuna hatua kubwa tumeifikia, hivyo tunaamini tutafanya makubwa zaidi kwenye mashindano yajayo.”

BOCCO, KOCHA ROBERTINHO WAFUNGUKA – ”KUNA SOMO TUMELIPATA, TULICHEZA MPIRA MZURI”…

Leave a Comment