×

Jumuiya Ya Wazazi CCM Temeke Yazindua Michuano Ya Wazazi Super Cup, Vijana Wafurika

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Temeke, Hamis Slim akitangaza kuzinduliwa kwa michuano hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Said Ally maarufu Asali ya Bibi.

Dar Es Salaam, 2 Juni 2023: Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Temeke inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Hamis Slim, jana Ijumaa imezindua michuano ya Wazazi Super Cup wilayani humo ambapo timu kutoka kata za wilaya hiyo zitatifuana kuwania kombe hilo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mwenyekiti wa ligi hiyo, Sunday Manara ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) amesema lengo la michuano hiyo ni kutafuta vipaji na kuleta hamasa kwa vijana kuungana pamoja kupitia chama cha Mapinduzi.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Fikiri Magoso (katikati) akifuatilia uzinduzi huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Temeke, Hamis Slim amesema pamoja na mambo mengine lengo la ligi hii pia ni kutekeleza ilani ya CCM katika kuendeleza michezo.

“Pamoja na kutekeleza ilani ya CCM lengo lingine ni kuwaweka vijana pamoja ili waendelee kuwa na imani na kuzidisha upendo kwa chama chao ili waweze kuwa wanachama bora wa CCM na kulijenga taifa imara na lenye nidhamu na nguvu kama kilivyo chama chenyewe.

Timu ya Mbagala ikikaguliwa kwenye uzinduzi huo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mbagala Rangitatu.

“Kwa kuangalia hilo ndiyo maana hata Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza nguvu nyingi sana katika michezo kama unavyoona hivi karibuni anavyoendelea kuzisapoti timu zetu katika michuano ya kimataifa.

“Na hivi tunavyoongea katika kuisapoti timu ya Yanga amewapa ndege mashabiki wa Yanga kwenda nchini Algeria kuishagilia timu hiyo katika mechi yake ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger hivyo nasi kwa levo yetu tunaimarisha michezo kwa kuanzia na ligi hii”. Alimaliza kusema Slim. HABARI/PICHA NA ISSA MNALLY/ GPL

Leave a Comment