
Dar es Salaam Juni 7, 2023: Mdhamini mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo imezindua kombe jipya la ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara lililoboreshwa. Kombe hilo ambalo lilizinduliwa mbele ya waandishi wa habari, litakabidhiwa kwa mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania mara kwa msimu huu na misimu ijayo.
Akiongea kwaniaba ya mkurugenzi mtendaji wa benki ya NBC, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa benki hiyo, Godwin Semunyu alisema benki ya NBC ikiwa kama mdhamini mkuu wa ligi imeboresha kombe kutokana na maoni ya wadau mbalimbali wa soka.

“NBC ikiwa mdhamini mkuu wa ligi ya Tanzania Bara inajivunia mafanikio makubwa ya ligi yetu. Kwasasa ligi yetu ni ya tano kwa ubora Afrika na hii ni hatua kubwa na nzuri kwa soka letu. Leo tumezindua kombe lililoboreshwa ikiwa pia ni sehemu ya kuongeza thamani kwa ligi yetu,” alisema.
Godwin aliongeza kuwa ikiwa ni sehemu ya maboresho ya ligi, benki ya NBC inatoa bima kwa wachezaji wote wa ligi kuu pamoja na familia zao na pia mikopo ya mabasi kwa timu zinazoshiriki ligi.

“Ili kuongeza hamasa kwa wachezaji na makocha, tunatoa tuzo mbalimbali kwa makundi haya kila mwezi. Benki ya NBC itaendelea kutoa mchango wake katika kusaidia maendeleo ya michezo hapa nchini kwakuwa inatambua umuhimu na mchango wa michezo kwa maendeleo,” aliongeza
Kwa upande wake mkurugenzi wa fedha wa bodi ya ligi Ibrahim Mwayela alisema udhamini wa NBC umekuwa wenye tija kubwa kwa ligi na kuongeza kuwa NBC ni mdau mkubwa katika maendeleo ya soka hapa nchini.

“Leo Tanzania tunajivunia ligi yetu kuwa moja katika ligi bora barani Afrika tukishikilia nafasi ya tano. Tunaishukuru sana benki ya NBC kwa udhamini wake ambao umesaidia kufika hapa tulipo huku tukisonga mbele kwa kujiamini,”alieleza.