
Dar es Salaam, 10 Julai 2023: Asasi ya Vibes Foundatin kwa kushirikiana na wabobezi wa matibabu ya afya ya akili kutoka hospitali mbalimbali ikiwemo Milembe ya Dodoma, Temeke, Amana, Muhimbili, kesho Julai 11 wanatarajia kuendesha kongamano kubwa lihusulo tiba ya afya ya akili ambapo vipimo na matibabu vitapatikana kutoka kwa madaktari hao bingwa.
Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa Family Vibes Foundation Dkt. Mayrose Kavura Majinge waratibu wa kongamano hilo aliwaomba wananchi wote kujitokeza kwenye kongamano hilo la bure linalotarajiwa kufanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar kuanzia saa kumi na mbili asubuhi mpaka saa nane na nusu jioni.
Dkt Mayrose aliendelea kusema;
“Family Vibes Foundation ni Asasi isiyo ya kiserikali inayoshughulika na huduma za Afya ya Akili-Kinga, Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii ambapo, huduma hizi hutolewa kwa kutumia Kliniki maalumu inayoitwa “Mahusiano & Family Clinic” inayohudumia mtu mmoja mmoja, vikundi, taasisi, watu walio katika mahusiano ya kifamilia na jamii kwa ujumla.
Ndugu waandishi wa habari
“Dhumuni la kuwepo hapa ni kuwafahamisha watanzania kuhusu Kongamano Tiba la kitaifa la afya ya akili ambalo litafanyika tarehe 11 Julai, 2023 kuanzia majira ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 8:30 mchana katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

“Katika kongamano hili tutakuwa na wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa lakini kutokana na unyeti wake, tumemualika Mkurugenzi wa hospitali ya Taifa Muhimbili kama mgeni rasmi na ni kutokana na ukweli kwamba tumeona umuhimu wa afya ya akili Kwa watanzania uelezwe kupitia kwa wenye taaluma yao.
Ndugu waandishi wa habari, katika kongamano hili mada kuu itakuwa ni “DHIBITI MAGONJWA YAKO KWA AFYA YA AKILI”.
Kwanini tumeona mada hii ndiyo muhimu katika kongamano hili?
Ndugu waandishi wa habari sisi ndiyo tupo kwenye taaluma kiasi kwamba kwa walioko nje wanaweza kuhisi moshi unaofuka lakini sisi tunaona moto wenyewe na jinsi unavyoteketeza jamii.
Hakuna ubishi na wala hakuna haja ya kuja na tafiti lakini wote mnajua hali ya afya ya akili kwa watanzania jinsi ilivyo.
Siyo siri, kila mmoja wetu hapa huenda amewahi kuona ama ofisini kwake au katika mitaa tunayoishi jinsi tatizo la afya ya akili linavyowaumiza watu.
Watanzania wengi wanashindwa kutimiza ndoto zao, wanashindwa kufanyakazi kwa ufanisi, wanadhuru, kujiua na hata kuua kwasababu tu ya afya duni ya akili.
Ndugu zangu watanzania, kwa mujibu wa takwimu za shirika la afyaduniani za mwaka 2017, 10% ya wafanyakazi hutumia muda wa kazi kwaajili ya Sonona na hii inasababisha ufanisi mdogo wa kazi na kama hili litaachwa hivi hivi umasikini utazidi kutuandama.
Aidha sababu za tatizo la afya ya akili ni nyingi lakini miongoni mwao ni pamoja na mtu kushindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, vinasaba, vilevi, magonjwa ya mwili, shinikizo la makundirika, msongo wa mawazo wa kiwango cha juu, unyanyasaji wa kijinsia, ukatili, kushindwa kuelewa na baina ya ndugu, mke na mume au wapenzi, aina ya malezi tunayowapa watoto wetu na migogoro. Vyote hivi vinasababisha afya duni ya akili.
Wengi wamekuwa wakihoji juu ya makundi yanayoathirika zaidi na baadhi ya takwimu zikionesha vijana ndiyo kundi kubwa lililo katika hatari, ni kweli, lakini niwafahamishe kuwa makundi yote ya umri na jinsia yanakumbwa na tatizo hili.
Kwa mfano, watoto wadogo, tunajua wazi kuwa hupokea hisia zinazofanana za mama hivyo nao huathirika ikiwa mama wajawazito watakuwa katika hali hiyo ndiyo maana tunasema kila kundi linaweza kukumbwa na change moto hii.
Ndugu Watanzania, hakuna changamoto inayokosa suluhu, afya duni ya akili inatibika kama tunavyoweza kutibu magonjwa mengine hospitalini.
Kupitia kongamano hili Tiba, njoo na familia yako katika uwanja wa Uhuru utaweza kupona au kumponyesha ndugu yako na jamaa yako na niwaambie ndugu zangu watanzania mbali na tiba katika kongamano hili kutakuwa na upimaji wa afya bure kama tulivyosema awali kwamba madaktari bingwa watakuwepo na watatoa huduma hizo.
Ndugu Watanzania nitoe wito kwenu, hatuwezi kuwa na Taifa Bora lenye uchumi imara, ikiwa tutalifumbia macho suala la afya duni ya akili.
Tuhakikishe tunafika katika kongamano hili muhimu sana katika mstakabali wa ustawi wa maisha yetu. Katika kongamano hili tutapata fursa ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoisumbua jamii yetu. Kwa tayari tumeshafanya mchakato wa kuwapata wafikiriaji ambao kwa karama zao watatusaidia kuchakata changamoto hizo na kutuletea suluhu. Miongoni mwa wafikiriaji hao ni pamoja na Mheshiwa Jumanne Kishimba na wenzake wenye uwezo wa kuleta mambo mapya na suluhu za changamoto za maisha.
Ndio kusema kongamono hili litadumu kwa miezi mitatu yaani litafunguliwa kwa kueneza uelewa kwa taifa kuhusu umuhimu wa elimu kwa afya ya akili ufunguzi utakaofanyika tarehe 11/7/2023 na litahitimishwa tarehe 9/10/2023 kuamkia siku ya afya ya akili duniani.
Ndugu Watanzania, licha ya kuwa kongamano hili litasaidia kutoa elimu kwenu ,litakuwa la aina yake kwani tutatoa fursa kwa mwenye maswali kuwauliza wataalam na hata mwenye maoni na mawazo chanya atapa fursa, lengo ni kuwa na Taifa bora lenye watu wenye afya bora ya akili.
Nitumie fursa hii Kwa mara nyingine tena kuwakaribisha watanzania wote katika kongamano hili pale katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 11 /07/2023 bila kusahau kuja na ndugu jamaa na marafiki ili tupone kwa pamoja.
Ahsanteni Kwa kunisikiliza, niwatakie maandalizi mema ya kuja katika kongamano hili. Mungu abariki mchakato wa Kongamano hili”. Alimaliza kusema
Dkt. Mayrose Kavura Majinge
Mkurugenzi Mtendaji
Family Vibes Foundation
Simu: 0783 885958
Barua pepe: [email protected]