
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephen Aziz Ki amefunguka kuwa sababu kubwa ya kufanikiwa kufunga bao katika mchezo wa juzi Jumatano ni kutokana na kufuata maagizo aliyopewa na na kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi kabla kuingia uwanjani.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Aziz Ki alifanikiwa kufunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam na kwenda fainali.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Aziz Ki alisema kuwa, kabla ya kuingia Gamondi alimwambia aende kusahihisha makosa kwa kuongeza presha kwa safu ya ulinzi ya wapinzani wao iliyokuwa ikifanya makosa mara kwa mara.
“Nimefurahi kufanya kile alichoniambia mwalimu kwa kuwa ananiamini na anataka nikacheza na kutumia nafasi ambazo tulikuwa tukizipoteza katika kipindi cha kwanza. Mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu ilikuwa lazima tupambane ili kuweza kupata matokeo.
“Mwalimu aliona sehemu gani wapinzani hawakuwa vizuri, ndiyo maana dakika 30 za kipindi cha pili tulifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 ambayo yamepatikana ndani ya dakika kumi za mwisho na kutupeleka fainali,” alisema Aziz Ki.