
Hatimaye mbio za hisani za Shule ya Sekondari ya St Mary Goreti ya Mjini Moshi zimewadia huku zikitarajiwa kufanyika Jumamosi Agosti 26.
Mkuu wa shule hiyo, Sr Clementina Kachweka alisema mipango yote imekamilika na mbio hizo na matembezi ya Km 10 na Km 5 zitafanyika katika Uwanja wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi.
“Tumeanza kugawa namba za kukimbilia Leo hii Alhamis Agosti 24 na zoezi litaendelea kesho Ijumaa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni,” alisema.
Alisema mbio hizo na matembezi ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa Kwa shule ya St Mary Goreti.
“Mbio hizi zinatumika kuhamasisha uchangishaji wa fedha Kwa ajili ya ukarabati wa majengo kabla ya sherehe za Jubilee,” alisema na kuongeza kuwa wanatarajia kukusanya Tsh milioni 600 kuwezesha ukarabati huo.
Alitoa wito Kwa wakazi wa Moshi na mikoa ya jirani wajitokeze kwa wingi kuchukua namba ili washiriki katika mbio za Jumamosi.
Kuhusu ratiba, alisema mbio hizo zitaanzia katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi saa kumi na mbili asubuhi ambapo zitaanza mbio za Km 10 na kufuatiwa na za Km 5.
Pamoja na mbio kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na mziki.
Kwa mujibu wa Sr Clementina, Kwa ambao hawataweza kushiriki mbio, wanaweza kuchangia Kwa kutumia Lipa namba ya Kampuni ya Tigo 7945925 na Vodacom 5301408.
“Tunafahamu wengine wako nje ya nchi, wengine wametingwa na majukumu lakini munatamani kuchangia. Naomba mtume michango yenu kwenye namba hizo hapo juu,” alisema. Shule ya St Mary Goreti ilianzishea mwaka 1999 hivyo mwakani itaadhimisha miaka 25.