
Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, Kipchumba Murkomen, amewafukuza kazi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA), Alex Gitari na Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Anga, baada ya kukatika kwa umeme kulikowaacha abiria wakiwa wamekwama gizani kwa saa kadhaa katika Uwanja Mkuu wa Ndege jijini Nairobi wa Jomo Kenyatta (JKIA)
Waziri Murkomen aliomba radhi kwa tukio hilo na usumbufu wote uliotokea. Naye Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta ameshushwa cheo na kuhamishiwa Uwanja wa Ndege wa Mombasa.
Japokuwa baadhi ya maeneo yamekwishapata umeme, majumba na biashara kadhaa katika sehemu nyingi za nchi bado zimeathirika na tatizo hilo lilioanza jana.

Katika mitandao ya kijamii wananchi wa Kenya wameshikwa na hasira kuwa Uwanja Mkuu wa Ndege haukuwa hata na Jenereta zilizokuwa zikifanya kazi.
Waziri Murkomen ameeleza kuwa Jenereta mbili zilinunuliwa miaka miwili iliyopita kwa ajili ya uwanja huo, hata hivyo hadi sasa bado hazijafungwa, na hakuna maelezo kamili juu ya hilo.
Wakati huohuo, kumekuwepo na foleni ndefu na hali ngumu katika milango mikuu ya kuingilia kwenye mbuga kadhaa za wanyama baada ya kufeli kwa mfumo wa kidigitali wa kufanyia malipo.
Kukatika kwa umeme sio jambo la ajabu nchini humo lakini kukatika kwa muda mrefu kwenye sehemu nyingi za nchi na haswa kwenye uwanja mkubwa wa Ndege jijini Nairobi, Hospitali kadhaa na hadi Ikulu kuwa gizani si jambo la kawaida.