×

Micho Aiombe Radhi Tanzania, Hajui Mapambano Iliyopitia Stars …

 

KOCHA Mkuu wa Uganda, Sredejovic Milutin ‘Micho’, nimeona anaweweseka kwa muda sasa tokea Tanzania kufanikiwa kufuzu AFCON 2023 nchini Ivory Coast.
Micho raia wa Serbia, alikuwa na matumaini makubwa kuwa kikosi chake cha Uganda kingeweza kufuzu kucheza AFCON na si Tanzania.
Matumaini makubwa aliyapata baada ya ushindi wa Uganda wa bao 1-0 jijini Dar es Salaam. Kabla ya mchezo huo, Taifa Stars ilikuwa imeitwanga Uganda kwa bao 1-0 ugenini.
Mechi ilichezwa mjini Ismailia, Misri kwa kuwa Uganda walikuwa wakitumia kama uwanja wa nyumbani. Wao wakalipa kisasi Dar es Salaam, siku ambayo Stars ilikuwa inahitaji sare pekee kufuzu AFCON.
Ajabu, baada ya hapo Micho amekuwa akiweweseka na kuishambulia Tanzania kwenye vyombo vya Habari na kitu anachokitumia ni kwa kuwa tu Tanzania ina kocha mwenye uraia wa Algeria.


Amekuwa akisema Tanzania na Algeria walipanga Tanzania ipate pointi moja kwa kuwa wana kocha Mualgeria. Tena anaongeza kusema Tanzania haikustahili kufuzu na badala yake Uganda kwa kuwa wana kikosi bora zaidi.
Angalia hapa, kikosi bora anapima kupitia nini. Kama ni head to head kati ya Tanzania na Uganda, kila mmoja kashinda kwa bao 1-0 dhidi ya mwenzake, nyumbani kwa mwenzake.
Baada ya hapo, Tanzania imekusanya pointi nyingi kuliko Uganda na ndio maana imefuzu AFCON. Uganda inaizidi nini Tanzania?
Achana na hivyo, Micho angekuwa na kikosi bora asingekuwa na shida ya kupambana na Tanzania mwishoni. Na utaona, Tanzania ilipata nafasi mbili za kufuzu na mwisho ikawa na nafasi kubwa zaidi ya Uganda.
Nafasi ya mwanzo, Tanzania ilitakiwa kupata sare tu dhidi ya Uganda jijini Dar es Salaam na kazi ingekuwa imeisha. Angalia, Uganda walishinda lakini hawakuwa wamefuzu.
Mechi za mwisho, Tanzania ilihitaji sare, Uganda ilitakiwa kuwa na vitu viwili ili kufuzu AFCON. Kwanza kushinda dhidi ya Niger jambo ambalo walifanikiwa kushinda kwa mabao 2-0 na kuiombea Tanzania ifungwe, jambo ambalo halikuwezekana.
Tanzania ilitakiwa sare au kushinda ugenini, Uganda ikitakiwa kushinda na kuomba dua mbaya kwa Tanzania. Maana yake, zaidi iliitegemea Algeria kuisaidia kufuzu.

Leave a Comment