
UOGONZI wa Simba umeweka wazi kuwa kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos watamalizia kazi waliyoianza Zambia.
Ni Oktoba Mosi, Simba chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ina kibarua cha kusaka ushindi baada ya mchezo waliocheza ugenini ubao kusoma Power Dynamos 2-2 Simba na Jumapili hii watacheza mchezo wa marudiano pale Dimba la Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Dar.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wachezaji wapo tayari na benchi la ufundi linazidi kuwapa mbinu ili wapate matokeo mazuri.
“Ni mchezo mkubwa na muhimu kwetu ukizingatia kwamba tunakwenda kucheza na timu yenye wachezaji wenye uzoefu na wanahitaji ushindi kama ambavyo sisi tunahitaji.
“Lakini sisi tutakuwa nyumbani, tulipowafuata kile tulichotarajia ambacho ni ushindi tulikosa hivyo wanakuja hapa tunawakaribisha nasi tunakwenda kumalizia kazi ambayo tuliianza tulipowafuata kwao,” alisema Ally.
Mshindi wa jumla kwenye mchezo wa Oktoba Mosi atatinga hatua ya makundi ambapo Simba wanapaswa kushinda mchezo huo bila kuruhusu nyavu kutunguliwa kutimiza malengo ya kutinga hatua ya makundi.
Stori na Lunyamadzo Mlyuka