
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amefika kata Murusagamba wilayani Ngara Mkoani Kagera kufatia agizo alilopewa na Naibu waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Dotto Biteko Septemba 29, mwaka huu la kuleta suluhisho la upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
Aweso amesema kuwa kufatia agizo la Dkt. Biteko tayari wizara ya Maji imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Murusagamba na kumtaka mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi kutumia wafungwa kuchimba mitaro ili ndani ya siku 30 mradi huo uwe umekamilika na kukabidhiwa kwa wananchi.
Amesema kuwa kutokana na watu kuongezeka katika kijiji cha Murusagamba kumepelekea huduma ya maji kuwa hafifu hivyo mradi huo unakwenda kupanuliwa na kuwekewa miundombinu mipya hili maji yawafikie wananchi kwa urahisi.
Aidha waziri Aweso amemuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kagera kutangaza mradi wa maji wa kijiji cha Ntanga wenye gharama Zaidi ya shilingi milioni 700 ili wananchi wa kijiji hicho waanze kunufaika na maji.
Sambamba na hayo ameagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Kumubuga kufika ofisi za mkuu wa wilaya kutoa maelezo ya lini anamaliza mradi anaoujenga kutokana na kuchelewa kwa mradi huo.