
HALMASHAURI ya Jiji la Tanga limetoa shukrani kwa Shirika la Amend baada ya kukamilisha mradi wa Usalama Barabarani kupitia Mradi wa ‘Tanga Yetu’ ambao umewezesha wananchi wa Jiji hilo kupata elimu ya kutosha kuhusu usalama barabarani sambamba na kuboresha miundombinu katika shule za msingi.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mradi huo ambao ulianza mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2023, Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow amesema katika kipindi cha miaka minne wamekuwa na Amend na kushirikiana kuhusiana na suala zima la usalama barabarani.
“Amend ni miongoni mwa mashirika yanayofanya kazi kwa ukaribu katika program ya ‘Tanga Yetu’, ni miongoni mwa miradi 17 tuliyokuwa nayo katika miradi ya ‘Tanga Yetu’ na moja ya mradi huo ni mradi wa usalama barabarani.Katika mradi huu waliokuwa wamepata kazi ya kuusimamia na kuendesha ni Amend.

“Mradi huu umefika mwisho na umefanyika kwa miaka minne ukiwa unafadhiliwa na Shirika la Botna chini ya mradi wa ‘Tanga yetu’ na leo tumekuja kuwapa taarifa wadau tuliokuwa tunashirikiana nao tangu mwanzo.
“Ni mradi ambao umekuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka hii minne kwa kuhakikisha elimu ya usalama barabarani imetengamaa na imejitosheleza katika jiji letu la Tanga, kwasababu mradi huu pia uligusa uboreshaji wa miundombinu,”amesema Shiloow.

Amefafanua kuwa, wameboresha miundombinu katika za msingi ikiwemo; Shule ya Msingi Usagara, Shule ya Msingi Chuda, Shule ya Msingi Mwazange na Shule ya Msingi Mabawa.
“Tumeboresha miundombinu hii ambayo imetengenezwa maeneo mahususisi ambayo watoto wanaweza kupita kwa usalama na kuepuka kupata ajali za barabarani.
“Lakini kuweka alama za barabarani, tumeweka matuta, kingo, zebra na alama mbalimbali za kuashiria watumiaji wa vyombo vya moto kwamba wako katika maeneo ya shule.
Ameeleza kuwa, Amend pia wametoa elimu kubwa kwa watoto wa shule za msingi, sekondari, madereva wa bodaboda, maofisa wa maendeleo ya jamii na Askari wa kikosi cha usalama barabarani.
“Elimu hiyo imetolewa vya kutosha katika Jiji la Tanga na zimetolewa kwa nyakati tofauti lakini hawakuishia hapo wametoa elimu kwa madereva zaidi ya 900 ambao nao walipewa elimu sahihi ya matumizi ya barabara lakini jinsi gani ya kumlinda mtumia barabara ili na yeye awe salama.” Ameeleza.
Ameongeza kikubwa zaidi ambacho Amend walikifanya na kuvutia zaidi ni kuanzisha Mahakama Kifani ya Watoto iliyokuwa ikiendesha kesi za madereva waliovunja sheria za usalama barabarani na madereva hao walihukumiwa.
Meya Shiloow amesema, Mahakama ya Watoto imewasaidia watoto hao kuwa na ujasiri na kufahamu haki zao kuwa sheria za barabarani zipo na zinatakiwa zifuatwe na zinaweza kutolewa hukumu na watu wakahukumiwa. Pia amesema kupitia mradi huo kumekuwepo na mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uelewa wananchi.
“Tunawashukuru Amend walitutengenezea mpango kazi wa Jiji letu la Tanga kuhusu suala zima la usalama barabarani, ni suala kubwa kwetu.Niwaambie tu Amend wamekuwa na sisi kwasababu tu ya kufadhiliwa na Fondation Botnar na sasa mradi umekwisha.
“Jambo la kufurahisha mradi huu umekwisha lakini Amend wamepata mfadhili mpya ambaye ni Serikakali ya Uswiss ambao wameona umuhimu wa kuendelea na Amend katika Jiji la Tanga pamoja na Jiji la Dodoma ambako nako watapata huduma kama ambazo zimetolewa kwetu.
“Amend wanafanya kazi kwa uhalisia na linafanya kazi na watu wenye uhitaji, watu ambao wanahitaji kusemewa na sisi kama viongozi wa Umma tunawasemea watoto wetu ili tujenge Taifa nzuri lisilokuwa na watoto wenye ulemavu kwa miaka ijayo na ili tujenga taifa lenye upendo ni lazima tuwajali hawa watoto ikiwa pamoja na kuangalia usalama wao,”amesema Shiloow.