
MWABA Dickson Job, beki wa kazi ndani ya kikosi cha Yanga, amemtuliza mazima Che Malone Fondoh wa Simba kwenye kuzuia hatari katika lango ndani ya mechi tano ambazo ni sawa na dakika 450.
Job ni chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga chini ya Miguel Gamondi, anashikilia rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufunga bao kikosini hapo msimu wa 2023/24 katika Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC.
Mbali na kufunga, nyota huyo kampoteza Che Malone kwenye idadi ya mabao ya kufungwa katika mechi hizo tano msimu huu.

Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imeokota nyavuni mabao mawili pekee ambayo yote ni dhidi ya Ihefu, ubao wa Uwanja wa Highland Estate uliposoma Ihefu 2-1 Yanga.
Kwa upande wa Simba, ukuta wao unaoongozwa na Che Malone kwa sasa, umetunguliwa mabao manne, huku beki huyo akiwa hajapata zali la kufunga.
Mchezo wa kwanza msimu wa 2023/24 ugenini, mabao mawili alishuhudia yakiwa ndani ya nyavu dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha mechi mbili zilizofuata za ugenini mfululizo waliokota bao mojamoja, dhidi ya Tanzania Prisons na Singida Fountain Gate.