×

Vijiji 9,671 vyafikishiwa maji

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso amesema kufuatia matokeo ya Tathimini ya Hali ya Upatikanaji wa Maji Vijijini katika Vijiji 12,314 iliyofanywa na Wizara ya Maji, na kupelekea kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini-RUWASA, Wizara imefanikiwa kupeleka maji katika vijiji 9,671 na vijiji vilivyobaki 2,643 vitakamilika ndani ya miaka miwili ijayo.

Aweso amemuhakikishia Rais kuwa Vijiji vyote vilivyobaki vitapata maji na Wizara itahakikisha visima na mabwawa yanachimbwa katika maeneo yote yenye uhitaji.

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji wa chanzo cha Ziwa Victoria, Aweso amemuhakikishia Rais mradi huo unatekelezwa kwa kasi na kesho tarehe 17/10/2023 ataenda kuzindua Mradi wa maji wa chanzo hicho wa Tinde – Shelui.

Aidha, Aweso amesema Mradi Mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaendelea kutekelezwa, ikiwa ni sehemu ya matunda ya Ziara yake nchini India na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kabisa adha ya maji kwa maeneo hayo.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anashiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkoa wa Singida katika Uwanja wa Bombadia, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku tatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani Singida.

Leave a Comment