×

Waziri Mkuu Awataka Madereva Wa Serikali kuzingatia Sheria za usalama barabarani

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka madereva wa Serikali kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote kwa sababu kuendesha gari ya Serikali haimaanishi wamepewa rungu la kuvunja sheria bali wanapaswa kuwa mfano wa kuzizingatia hasa zile za usalama barabarani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, “ukiwa dereva wa Serikali haimaanishi kuwa uko juu ya sheria bali kila dereva anatakiwa kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote. Aidha, madereva wa vyombo visivyo vya Serikali wanapaswa kujifunza kutoka kwenu madereva wa Serikali.”

Pia, Waziri Mkuu amesema madereva hao wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ya madereva wa Serikali ambayo yanawataka madereva hao kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani. “Madereva wa Serikali hakikisheni mnakuwa kioo cha jamii.”

Ameyasema hayo Jumanne, Oktoba 24, 2023 alipofungua Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali, katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro. Kongamano hilo limebeba kauli mbiu isemayo; “Dereva wa Serikali bila ajali inawezekana. Kazi iendelee”

Akizungumzia kauli mbiu hiyo, Waziri Mkuu amesema ni kweli inawezekana kuendesha magari ya Serikali bila kusababisha ajali iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria zilizopo, hivyo amewasisitiza madereva hao wahakikishe wanafuata sheria.

“Ninawapongeza sana kwa kuwa kaulimbiu hii pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 105 (K) ambayo inailekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine kuendelea na jukumu la kudhibiti ajali za barabarani.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeshafanya jitihada kubwa katika kutatua kero za watumishi wa kada hiyo ya udereva na bado inaendelea kuzitatua changamoto zinazojitokeza kwa kushirikiana na Chama chao.

Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na itaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda maslahi ya madereva wa Serikali pamoja na kuyafanyia kazi maombi na ushauri utakaotolewa.

Live: PASUA KICHWA! UTEUZI wa MAKONDA, WAGAWA VIGOGO/ CCM WAHUJUMIANA/ KESI AKINA MDEE MBELE TENA

Leave a Comment