
VYAMA vya siasa vimehimizwa kushiriki kwenye majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kufanyika katika Kata za Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele ametoa wito huo leo tarehe 16 Novemba, 2023 wakati akifungua mkutano wa Tume na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam.

“Vyama vya siasa kwenye zoezi hili vitashiriki kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika wakati wa majaribio ya uboreshaji wa Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.
Amenongeza kuwa majaribio ya uboreshaji yanafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe zitakazopangwa na kutangazwa na Tume.

Majaribio ya uboreshaji yatahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kundi lingine litakalohusika kwenye zoezi hili ni; wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.

Majaribio ya uboreshaji yatafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura. Kati ya hivyo, vituo 10 ni vya Kata ya Ng’ambo na vituo sita (6) ni kutoka Kata ya Ikoma. Vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
“Tume inatoa wito kwa wakazi wa Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika majaribio ya uboreshaji wa Daftari na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa,” amesema Jaji Mwambegele.