
SERIKALI kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanmyakazi (WCF) imetangaza Fao jipya la Huduma ya Utengemao wa Kijamii (Social Rehabilitation) kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi na hivyo litawaongezea faraja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amesema.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Novemba 29, 2023, alipokutana na wanufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani inayotarajiwa kufanyika kitaifa jijini Dodoma, Desemba 2, 2023, amesema “Ndugu zangu hivi karibuni tutaanza kutoa Fao la Huduma ya Utengamao wa Kijamii na kutoa mafunzo ya kujenga ujuzi kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu wakiwa kazini na aina ya ujuzi tutakaotoa utategemea uhitaji.” Alisema

Alisema lengo la Serikali ni kumpatia mfanyakazi ujuzi ambao utaendana na hali ya ulemavu wake, mfano alikuwa dereva na akapata ajali iliyopelekea ulemavu wa miguu, huyu anaweza kubadilisha ujuzi na kusomea kazi nyingine.
Sambamba na kuwajengea ujuzi, fao hilo pia litatoa fursa ya kumjengea miundombinu inayoendana na hali yake, na hivyo kumuwezesha kumudu maisha katika mazingira anayoishi.” Alifafanua Profesa Ndalichako.
Kwa upande wao, wanufaika wa WCF wameishukuru Serikali kwa huduma wanazopokea kutoka katika Mfuko huo licha ya kupata ulemavu na wengine kuondokewa na wapendwa wao.
“Naomba kuhamasisha waajiri kuweza kuwachangia wafanyakazi wao, kwani viwango vya uchangiaji ni vidogo, tunaishukuru Serikali imepunguza viwango vya uchangiaji hadi kufikia asilimia 0.5” Alisema Norbert Tesha, ambaye amepata ulemavu wa kudumu baada ya kupata ajali akiwa kazini mwaka 2016.
“Hatuwezi kujua kesho yetu, lakini kama kuna misingi mizuri iliyowekwa leo, basi kesho yetu itakuwa njema, kila mtu ni mlemavu mtarajiwa.” Alisema, Bw. Tesha.

Mnufaika mwingine Bi. Emmaculet Nhigula, ambaye alimpoteza mumewe kwa ajali ya gari, amesema, “Mimi na watoto wangu wanne, tunanufaika sana na Mfuko huu, rafiki yetu kwa sasa ni WCF, huwa nikipita kwenye barabra hii na kuliona jengo lenu, ninasema hawa ni rafiki zangu wanaotembea na mimi nyakazi ngumu.” Alisema
Alisema yale mafao ya kila mwezi yamekuwa na msaada mkubwa sana, yamesaidia kusomesha watoto wangu na sikuweza kuwahamisha kutoka shule walizokuwa wanasoma kabla ya kufariki baba yao.” Alisema Bi. Emaculate.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, yanalenga kuwahamasisha viongozi wa taasisi za kibiashara Duniani kutambua mchango maridhawa wa watu wenye ulemavu.
Kwamujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwasasa inakadiriwa kuwa watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na changamoto ya ulemavu, hii ni sawa na asilimia 16% ya Watu wote duniani.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “ Tuungane katika hatua za Kuokoa na kufikia Malengo ya SDGs kwa Watu wenye Ulemavu”.

