×

Tanzania Yatajwa Kuwa Kinara Kwa Kudhibiti Mianya ya Uvujaji Mitihani

 

TANZANIA imetajwa kuwa miongoni mwa nchi kinara kwa kudhibiti mianya ya uvujaji mitihani.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolfu Mkenda wakati akifungua maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) yaliyobebwa na kauli mbiu isemayo ‘Upimaji wa umahiri kwa misingi ya haki suluhisho la ajira karne ya 21’.
Mkenda alisema pamoja na kuwepo na changamoto mbalimbali za wizi wa mitihani lakini Tanzania ipo vizuri kudhibiti mianya hiyo kuliko nchi nyingine.
“Ninalipongeza Baraza la Mitihani Tanzania kwa kampeni mliyoianzisha ya kuzuia wizi wa mitihani, mbali na changamoto iliyopo bado Tanzania tupo vizuri kudhibiti wizi wa mitihani  ukilinganisha na nchi nyingine,”alisema.
 Profesa Mkenda alisema mtu akishiriki katika wizi wa mitihani anakuwa anaharibu maadili ya mtoto hivyo alishauri walimu wakiwashindanisha wanafunzi wao wahakikishe hawahusiki na wizi huo.
“Huwa nasikitika kusikia wizi wa mitihani ukihusisha walimu na baadhi ya viongozi nawaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na kamati za mitihani mnaposhindanisha shule mtumie miongozo iliyowekwea na msishindanishe kwa kuhamasisha wizi wa mitihani,” alisema.
MIMBA SHULENI
Profesa Mkenda alisema wizara inatarajia kufanya kampeni nchi nzima kuhamasisha mtoto kujilinda zaidi kwa lengo la kuondokana na wimbi la wanafunzi kupata mimba shuleni na kushindwa kutimiza malengo yao.
“Tunasikitika kuona idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha darasa la kwanza sio wanaohitimu darasa la saba hivyo tutafanya utafiti   na kubaini mikoa ambayo ni tatizo kwa sababu hatuwezi kuvumilia wale waliojiandikisha darasa la kwanza hawamalizi shule,” alisema.
Pia amewataka walimu kuhakikisha michango wanayoichangisha shuleni isiwe kikwazo cha wanafunzi kushindwa kwenda shule ndio maana serikali imefuta ada.
KATIBU MTENDAJI NECTA
Naye Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed alisema   wamejipanga kikamilifu kutekeleza mabadiliko ya sera ya elimu na mitaala mipya.
Alisema  NECTA inatarajia kufanya upimaji  utakao weza kubaini uwezo wa kufikiri na kutenda ambao utaendana na  mabadiliko ya sera.
Akizungumzia miaka 50 alisema mafanikio yaliyopo  yamewezekana kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini.
 “Katika kuadhimisho miaka 50 tulifanya kongamano  la Kitaaluma Zanzibar, kupanda miti nchini kwa kuwa NECTA ni watumiaji wakubwa wa karatasi,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba aliahidi kushirikiana na  NECTA katika  kudhibiti  vitendo vya udanganyifu wa mitihani  vinavyotendwa na  baadhi  ya watu.

Leave a Comment