
Mahakama ya Juu ya Colorado imeamua kuwa Donald Trump hawezi kugombea urais mwaka ujao katika jimbo hilo, ikinukuu kifungu cha katiba kuhusu uasi.
Katika uamuzi wa kihistoria, mahakama iliamua 4-3 kwamba Bw Trump hafai kuwa mgombeaji.
Ni mara ya kwanza kwa Kifungu cha 3 cha Marekebisho ya 14 ya Katiba ya Marekani kutumika kumuondoa mgombea urais.
Majaribio kadhaa ya kumtimua Bw Trump kwenye kura katika majimbo mengine yameshindwa.
Uamuzi wa Jumanne – ambao umesimamishwa kusubiri rufaa hadi mwezi ujao – hautumiki kwa majimbo nje ya Colorado.
Uamuzi huo unatumika tu kwa uchaguzi wa mchujo wa jimbo tarehe 5 Machi, wakati wapiga kura wa chama cha Republican watamchagua mgombea wao wa urais wanayempendelea, ingawa inaweza kuathiri uchaguzi mkuu mwezi Novemba.
Majaji waliandika katika hukumu yao: “Hatufikii uamuzi huu kirahisi. Tunazingatia ukubwa na uzito wa maswali yaliyo mbele yetu sasa.
“Sisi vile vile tunazingatia wajibu wetu mzito wa kutumia sheria, bila woga au upendeleo, na bila kushawishiwa na maoni ya umma kwa maamuzi ambayo sheria inatuagiza kufikia.”
