
Mtoto wa Msanii wa Bongo Fleva Shetta, Qailah Nurdin Bilal amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi Taifa katika Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa 9 wa Chipukizi Taifa uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Qayllah ameshinda kwa kupata kura 303 kati ya kura halali 429 zilizopigwa huku akiwashinda wenzake watatu aliokuwa akishindana nao.
Chama Cha Mapinduzi kimempongeza Komredi Qaillaha Nurdin Bilal kwa kuchaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chipukizi wa CCM 2023 kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi wa CCM Taifa.

Simba Jerry Silaa mtoto wa Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Uendeshaji Chipukizi Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Tanzania Bara akiwashinda wenzake wanane.
Katika uchaguzi huo uliofanyika ndani ya mkutano wa tisa wa Chipukizi Taifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Simba Jerry Silaa aliongoza kwa kupata kura 155 kati ya 431 zilizopigwa.
Isack Mwigulu Nchemba ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Iramba na Waziri wa fedha amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza kuu la UVCCM Taifa kutoka Tanzania Bara katika mkutano wa tisa wa Chipukizi Taifa uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Isack amepata kura 118 kati ya kura 433 zilizopigwa huku moja ikiharibika ambapo amewashinda wenzake tisa (9) katika kinyang’anyiro hicho.