
NEEMA inazidi kuwaangukia yanga kwani taarifa njema kwao ni winga wa Lupopo FC, Manu Labola Bota ameweka wazi kutamani kukipiga ndani ya mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara.
Winga huyo kwa sasa mkataba wake na klabu hiyo upo ukingoni jambo ambalo linamfanya kuwa na maamuzi ya kujiunga na timu yoyote ambayo itafikia makubaliano na uongozi wake.
Akizungumza na Spoti Xtra, bosi mpya wa mchezaji huyo, Faustino Mukandila ameweka wazi kuwa winga huyo anatamani kuichezea ligi ya Tanzania hususani Yanga huku akifurahia kumpata mchezaji huyo na kuwa msimamizi wake mapema ndani ya mwezi huu.
“Ni kweli uongozi wetu wa Bro Soccer Management tumefanikiwa kumuongeza mmoja kati ya mawinga bora kwa sasa ndani ya ligi ya DR Congo, Manu Labota, hivyo kwa sasa kampuni yetu tunammiliki mchezaji huyu.
“Tunafahamu huu ni muda wa tetesi lakini pia ni muda wa usajili kwa baadhi ya nchi lakini kwa upande wa mchezaji amegusia kutamani kucheza ligi ya Tanzania pia ameitaja Yanga kuwa anavutiwa nayo, lakini hii haimaanishi kuwa atacheza huko au atajiunga huko. “Hii sio kwake tu, kuna wachezaji wengi ulaya wanatamani kucheza Real Madrid au Barcelona lakini unakuta hawajawahi na hawakufanikiwa kucheza licha ya wao kuwa katika timu nyingine kubwa za Ulaya,” alisema Faustino Mukandila.
Na Marco Mzumbe
