
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeujulisha Umma kuwa ndege yake aina ya Q300 (Bombardier) iliyopo kwenye matengenezo nchini Malta sio miongoni mwa ndege mpya zilizonunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha Mpango wa Ufufuaji wa ATCL ulioanza kutekelezwa mnamo mwaka 2016.
Taarifa ya Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha ATCL kwa Umma imebainisha kuwa ndege hiyo haikununuliwa na Serikali bali ni miongoni mwa ndege mbili zilizopatikana kupitia mbia aliefanya uwekezaji kwa kuleta ndege mbili za aina ya Dash 8-Q300 mwaka 2008 na kupewa usajili wa namba 5H-MWG na 5H-MWF kwa kufuatana.
ATCL imeongeza kuwa Ndege hizo za Q300 ziliundwa mnamo mwezi Mei 1997 na kabla ya kuwasili nchini zilikuwa zimetumika kwa takribani miaka 11. Hata hivyo, Kampuni ya Bombardier (Manufacturer) ilisitisha uundwaji wake tangu Mei 2009.
“Ndege zilizonunuliwa na Serikali kuanzia mwaka 2016 ni ndege kumi na tatu (13) ambazo ni Q400 – Bombardier (5), Airbus A220-300 (4), Boeing 787-8 (2), Boeing 767-300F (1) na Boeing 737 MAX-9 (1).” imesema taarifa hiyo.
“ATCL ilibakiwa na ndege ya Q300 moja yenye usajili wa namba 5H-MWF baada ya ndege yenye usajili wa namba 5H-MWG kupata ajali mwaka 2012 na kushindikana kutengenezeka kutokana na ukubwa wa uharibifu wa ndege hiyo.”
“Ndege iliyobakia iliendelea na safari zake hadi mnamo Mei 2017 baada ya waundaji (Manufacturer) wa ndege hizi kuagiza kuwa ndege zote za aina hii duniani zisiendelee na safari hadi zitakapofanyiwa matengenezo ya lazima ya matenki ya mafuta kwa ajili ya usalama.”
“Sanjari na agizo hilo, Ndege hii pia ilihitaji kufanyiwa matengenezo makubwa yanayojulikana kitaalamu kama “6C-Check” ambapo ilifika nchini Malta mwezi Novemba 2020 kwa ajili ya matengenezo hayo.” imesema ATCL.
Aidha, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa vipuri iliyosababishwa na athari za UVIKO 19 ambapo wazalishaji wa vipuri walipunguza na wengine kuacha utengenezaji wa vipuri kumesababisha matengenezo hayo kutokamilika kwa muda uliotarajiwa. Ndege hii inatarajiwa kurejea nchini baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo.

