
Michuano ya AFCON 2023 inaendelea kurindima leo Januari 21, 2024 kwa mechi tatu za hatua ya makundi huku timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikiendelea kusaka ushindi wa kwanza kwenye fainali tatu za AFCON ilizoshiriki mpaka sasa.
Stars iliyopo chini ya Kaimu kocha mkuu Hemed Morocco akisaidiana Juma Mgunda itakuwa na kibarua dhidi ya ‘Chipolopolo’, Zambia katika dimba la Laurent Pokou, San Pedro Nchini Ivory Coast majira ya saa mbili kamili usiku.
Kwingineko Morocco watachuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo majira ya saa 11:00 jioni katika dimba la Laurent Pokou, San Pedro huku Afrika Kusini ikipimana nguvu dhidi ya Namibia majira ya saa 5:00 usiku dimbani Amadou Gon Coulibaly, Korhogo.