×

CMSA Yatoa Elimu ya Masoko ya Mitaji Kwa Nchi 16 za SADC

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus Mkama akizungumza na waandishi wa habari.

CoSSE imeanzishwa chini ya Kifungu cha 14 cha Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya SADC, ambapo pamoja na masuala mengine, inalenga kuboresha uendeshaji na uwezo wa kitalaam wa masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC; kukuza biashara na ukwasi katika masoko ya hisa; kubadilishana ujuzi na uzoefu miongoni mwa watendaji wa masoko ya hisa katika nchi wanachama wa SADC; na kuhamasisha mahusiano miongoni mwa washiriki katika masoko ya mitaji. Mkutano huu ni jukwaa muhimu katika kuchagiza kufikiwa kwa malengo haya.

kuhamasisha maendeleo endelevu ya masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC ni hatua muhimu katika kuwezesha uwekezaji
unaozingatia uwajibikaji; kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia miradi na biashara zinazokidhi misingi ya malengo endelevu;


kuimarisha uwazi wa masoko; kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi za ukanda wa SADC; na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. Hivyo basi, CoSSE inatarajiwa kutekeleza jukumu muhimu la kuhamasisha maendeleo endelevu kwa kuwezesha mikutano ya wadau; kubadilishana utaalam; na kuongeza ushirikiano miongoni mwa masoko ya hisa, mamlaka za usimamizi, watoa dhamana, wawekezaji na wadau wengine ili kuhakikisha masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, maendeleo ya jamii na utawala bora (ESG) yanaingizwa katika mipango ya maendeleo ya masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Masoko Mitaji na Dhamana (CMSA) imekuwa ikitekeleza
mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji ambazo zimewezesha kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na mauzo katika soko la hisa.

Thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 31.2 na kufikia shilingi trilioni 37.3 katika kipindi kilichoishia Januari 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 28.4
Katika kipindi kilichoishia Januari 2021; na mauzo katika soko la hisa yameongezeka kwa asilimia 61.6 na kufikia shilingi trilioni 9.3 katika kipindi kilichoishia Januari 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 5.8 katika kipindi kilichoishia Januari 2021.


Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji nchini Tanzania, ni pamoja na utoaji wa hatifungani ya kwanza ya Kijani yaani Green Bond yenye thamani kubwa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara
iitwayo "Kijani Bond" ambayo iliwezesha kupata shilingi bilioni 171.83 sawa na mafanikio ya asilimia 430, ambapo fecha zilizopatikana zinatumika kutekeleza miradi ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Aidha, utoaji wa hatifungani ya Jasiri Bond ambayo imewezesha kupata shilingi bilioni 74.2 sawa na mafanikio ya asilimia 297, umeweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza yenye mguso wa Jinsia yaani Gender Bond kutolewa katika Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Fedha zilizopatikana zinatumika kuendeleza biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanawake; na zile zinazomilikiwa na wanaume lakini zinazalisha bidhaa na huduma zinazomgusa mwanamke. Vile vile, masoko ya mitaji ya Tanzania yamefanikiwa kutoa hatifungani ya Jamii yaani Social Bond ambayo imewezesha kupata shilingi bilioni 212.9 sawa na mafanikio ya asilimia 284. Hatifungani hii imeweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza yenye mguso kwa jamii kutolewa katika ukanda wa
Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa imetolewa katika fedha za kigeni na za kitanzania yaani multicurrency. Fedha zilizopatikana zinatumika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na biashara endelevu kwa jamii.


Halikadhalika, katika jitihada za kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji zinazowezesha kupata rasilimali fedha za kugharamia miradi ya kuboresha miundombinu ya maji na uhifadhi wa mazingira, Mamlaka Masoko ya Mitaji Tanzania imeidhinisha waraka wa matarajio wa mauzo ya hatifungani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), yenye thamani ya shilingi bilioni 53.1.

Uzinduzi wa mauzo umefanywa na Mh. Dk. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Februari 2024 jijini Tanga.

Hatifungani hii imeweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza nchini Tanzania kutolewa na Taasisi ya umma yaani the first Subnational Water Infrastructure Green Revenue Bond.

Hatifungani ya Tanga UWASA ni hatifungani yenye ubunifu unaojumuisha vipengele vinavyogusa taasisi ya umma, ujenzi wa
miundombinu ya huduma endelevu za maji, utunzaji wa mazingira na miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara.

Aidha, hatifungani hii inaweka msingi madhubuti kwa taasisi zingine za umma na mamlaka za serikali za mitaa nchini Tanzania na katika ukanda wa SADC, wa namna ya kupata fedha za kugharamia miradi yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara kupitia
masoko ya mitaji.
Imelezwa kuwa mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa warsha hiyo, ambaye alikuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametoa pongezi za dhati kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kutekeleza hatua muhimu ambazo zinawezesha kufikia azma na malengo ya Serikali ya kuwa na uchumi shindani na endelevu kwa maendeleo ya watu.

Aidha ameongeza kuwa Mkutano huo utachangia zaidi katika maendeleo ya masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC. Natoa rai
kwa washiriki wote kutumia fursa ya mkutano huu kuongeza ujuzi na kupata uzoefu zaidi wa nanma ya kutekeleza mikakati inayochagiza maendeleo endelevu ya masoko ya mitaji katika ukanda wa SADC ili kuyawezesha masoko haya kuwa na thamani zaidi na kuweza kuvutia wawekezaji wa ndani na kimataifa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuleta maendeleo endelevu na kuimarisha uwekezaji katika masoko ya mitaji kwa mustakabali wa maendeleo katika ukanda wetu wa SADC, Afrika na Dunia kwa ujumla.

Leave a Comment